• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Total man mpya

Total man mpya

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah, ameonekana kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa zaidi huku akipigania na kutetea ajenda za serikali ya Kenya Kwanza nje na ndani ya Bunge.

Mbunge huyo wa Kikuyu anayehudumu muhula wa tatu amekuwa akiwakabili hata mawaziri na maafisa wakuu wa serikali kwa ujasiri, akiwataka kuwajibikia nyadhifa zao au kujiuzulu jinsi alivyokuwa akifanya aliyekuwa waziri Nicholas Biwott enzi za utawala wa chama cha Kanu.

Haya yalijitokeza wazi Jumatano wakati mwanafunzi huyo wa zamani wa shule ya wavulana ya Alliance, alipomkemea Waziri wa Vijana na Michezo Ababu Namwamba kwa kumtaka kutekeleza majukumu yake na kuyawajibikia.

Bw Ichung’wah, alimweleza Bw Namwamba asidhani kwamba, kazi yake kama Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa ni kutetea mawaziri.

“Nataka waziri huyu na wengine wafahamu vyema, kwa sababu baadhi yao wanaweza kuamini kimakosa kwamba kama kiongozi wa wengi, ninawakilisha mawaziri. Inapohusu masuala ya uwajibikaji, nitawakabili kama kiongozi wa walio wengi,” Bw Ichung’wah alimweleza Bw Namwamba.

Kabla ya waziri huyo kukubali wito wa kufika mbele ya Bunge la Kitaifa, Bw Ichung’wah alikuwa amemkashifu vikali kwa kutowajibika kikamilifu.

“Haukuteuliwa kuwa waziri katika nchi hii ili uwe ukipeperusha bendera katika barabara na kuruhusiwa kupita kwenye misongamano ukisindikizwa na magari aina ya Subaru. Uliteuliwa kuhudumia wanamichezo wa nchi hii,” alisema Ichung’wah akiwa Bungeni.

Alimkosoa vikali Bw Namwamba akisema hatengi muda wa kushughulikia wanamichezo wanaowakilisha nchi katika michezo ya kimataifa.

“Ni sharti waziri afike mbele ya Bunge hili na nitamfanya afike na aeleze hasa Bunge hili na watu wa Kenya kwa nini hana muda wa kushughulikia watu wa Kenya wanaowakilisha nchi yetu,” aliongeza.

Namwamba alitii, akafika Bungeni Jumatano na kuomba msamaha kwa kukosoa hatua ya kuitwa na kamati ya Bunge. hapo awali.

Nje ya Bunge, Bw Ichungwah amekuwa akichora taswira ya mwanasiasa asiyeogopa kutoa matamshi makali ya kukashifu na kukabili wanaokosoa serikali.

Mnamo Aprili 2023, mbunge huyo mwenye umri wa miaka 46, alijigamba kuwa ndiye anaweza kuruhusu handisheki na serikali ya nusu mkate kati ya serikali na upinzani na hangekubali kamwe.

“Iwapo kuna mkate wa kugawa, ni kati ya William Ruto (Rais) na Rigathi Gachagua (Naibu Rais). Ni mimi ninayeshika kisu na sitakubali,” Bw Ichungwah alisema akihutubu katika hafla ya kanisa la AIPCA, Limuru mnamo Aprili 6.

Mchanganuzi wa siasa John Kimotho anasema kwamba, Ichung’wah anajijengea nafasi katika historia ya Kenya inavyofanyika kila wakati utawala mpya ukiingia mamlakani.

“Mzee Kenyatta alikuwa na akina Mbiyu Koinange, Moi alikuwa na akina Biwott, Uhuru alikuwa na Matiang’i, na sasa Ichungwa’h ameibuka katika utawala wa Kenya Kwanza,” asema Kimotho,

Wakati wa kilele cha maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya mnamo Machi, Ichungwah alinukuliwa akionya kuwa mali ya familia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ingevamiwa akimlaumu kwa kufadhili upinzani kuzua vurugu.

“Ningetaka kumhimiza rais mstaafu kuheshimu mali ya watu. Iwapo hautafanya hivyo, na uvamie mali ya watu, pia tutavamia ardhi yako na kuhakikisha wale wasio na mashamba wanapata,” Bw Ichung’wah alinukuliwa akisema.

Mazungumzo ya pande mbili yalipozinduliwa, Ichung’wah ambaye anaongoza kikosi cha Kenya Kwanza alitisha upinzani kwa kusisitiza waahidi kutoitisha maandamano kabla ya kuketi katika meza ya mazungumzo.

Ichung’wah aliingia Bungeni mara ya kwanza 2013 na kwenye uchaguzi wa 2017 alihifadhi kiti chake cha eneobunge la Kikuyu, kaunti ya Kiambu bila kupingwa kabla ya kukishinda tena mwaka jana kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kuteuliwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto atarajiwa kuzindua miradi ya maendeleo eneo la...

Wafugaji ng’ombe wa maziwa Gatundu waelimishwa kuhusu...

T L