• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Uchovu walemaza kampeni za OKA

Uchovu walemaza kampeni za OKA

Na BENSON MATHEKA

VINARA wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA), wanaonekana kukosa msukumo wa kampeni japo wanasisitiza kuwa wameweka mikakati ya kushinda uchaguzi mkuu ujao.

Tofauti na Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambao wamekuwa wakifanya msururu wa mikutano ya kisiasa kuuza sera zao, vinara wa OKA, Musalia Mudavadi( ANC), Kalonzo Musyoka( Wiper) Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetangula wamekuwa wakifanya mkutano mmoja na kutoweka.

Mara ya mwisho vinara hao kuandaa mkutano wa hadhara ilikuwa mtaani Githurai, Nairobi mnamo Oktoba 31, siku mbili baada ya kukutana na wajumbe wa vyama vyao mjini Kakamega na kuhutubia wakazi.

Ingawa katika mikutano yao wakati huo waliahidi kutembelea maeneo tofauti kuuza sera zao, wamekuwa kimya huku kila mmoja akionekana kuendeleza shughuli zake kibinafsi kando na kampeni za siasa.

“Kuna wale wanaosema kwamba OKA inakutana kwenye kumbi. Leo, tumekuja kuwaambia kwamba tumejiandaa, kila kitu kiko tayari na meli imeondoka bandarini,” walisema wakiwa Kakamega mnamo Oktoba 28.

Mtindo wao wa kukosa kuzidisha kampeni, umefanya Wakenya kuhisi kwamba vinara hao hawana uwezo wa kifedha wa kuandaa kampeni za urais, wamekosa mikakati ya kushindana na wapinzani wao au hawako makini kugombea urais.

Mnamo Jumatatu, Bw Mudavadi alijitokeza baada ya kimya cha siku saba kilichoibua uvumi kuhusu afya yake. Ingawa alisema angali buheri wa afya, duru zilisema aliugua na kushauriwa na madaktari wake kupunguza kasi ya kampeni za kisiasa kwa muda.

“Niko mzima sana. Baada ya siku chache mtaniona,” Bw Mudavadi alisema Ijumaa. Bw Musyoka, Wetangula na Bw Moi hawajaonekana pamoja kwenye kampeni tangu mkutano wa vinara wote wa muungano huo mtaani Githurai waliposisitiza kuwa hawataunga au kukubali kushurutishwa kuunga mgombeaji urais nje ya OKA.

Mnamo Novemba 4, Bw Musyoka na Bw Moi walihudhuria kongamano la kitaifa la wajumbe wa Ford Kenya kabla ya kila mmoja kwenda njia yake.

Wadadisi wa siasa wanasema, vinara wa OKA hawana nguvu na mikakati kama ya Dkt Ruto na Bw Odinga ambao, mbali na kuwa na uwezo wa kifedha, wanajipanga kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Kile ambacho Bw Musyoka, Bw Mudavadi, Bw Wetangula na Bw Moi hawataki kusema ni kuwa, hawana uwezo wa kuendesha kampeni kama wapinzani wao. Inaonekana wazi kuwa Bw Odinga anaungwa na watu wazito wanaompangia mikutano yake.

Chama chake cha ODM pia kina nguvu za kifedha na mipango thabiti. Dkt Ruto pia amekuwa akikutana na wajumbe kutoka maeneo tofauti na kuandaa mikutano kadhaa ya kampeni kila siku inayogharimu mamilioni ya pesa,” asema mchanganuzi wa siasa David Awiti.

Anasema japo Bw Odinga ni mzee kuliko vinara wa OKA, amekuwa akimtoa jasho Dkt Ruto ambaye ni mdogo wake kwa miaka zaidi ya 20 kwa kuandaa mikutano mingi bila kuchoka. Vinara wa OKA walikuwa wametangaza msururu wa mikutano eneo la Pwani baada ya kuzuru eneo la Magharibi.

Kufikia wakati wa kwenda mitamboni jana, hawakuwa wametangaza ni lini watafanya hivyo. Bw Awiti anasema nguvu za kampeni hutokana na pesa, mipango na uungwaji mkono.

“Hakuna mwanasiasa anayeweza kutembelea eneo ambalo hatapata wafuasi wa kuhutubia hata kama ako na pesa. Unaweza kuwa na wafuasi eneo na ukose nguvu za pesa za kuwatembelea,” aeleza.

You can share this post!

DCI waahidi Sh10m kwa atakayenasa mshirika wa magaidi

Rio Ferdinand amtaka Solskjaer abanduke Man-United kabla ya...

T L