• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:07 PM
UDA yaanza kuiga makosa ya Jubilee

UDA yaanza kuiga makosa ya Jubilee

NA WANDERI KAMAU

MIVUTANO ya kisiasa iliyokiandama chama cha Jubilee inatishia kuchipuka upya katika chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA), kutokana na kauli za baadhi ya viongozi wake kwamba lazima vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza vivunjwe.

Ijapokuwa Rais Ruto anashikilia kwamba lazima vyama tanzu katika muungano huo vipewe uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ikiwa vitajiunga na UDA au la, msimamo wake ni kuwa sharti vyama hivyo vivunjwe.

Hilo lilidhihirika Ijumaa wakati wa mkutano wa Baraza la Kusimamia Chama (NGC), uliofanyika katika Ukumbi wa Bomas of Kenya.

Kwenye hotuba yake, Rais Ruto, ambaye ndiye kiongozi wa chama hicho, alisema lengo kuu la UDA ni kuwa chama kikubwa zaidi cha kisiasa, akisisitiza kuhusu haja ya vyama vitakavyoamua kujiunga nacho kuvunjwa.

“Tunataka idhini yenu (wanachama) tuzungumze na wao (vyama tanzu), ili tuwashawishi wale watakuja kuungana na sisi waje tuungane tuwe chama kikubwa cha kitaifa pamoja,” akasema Rais Ruto, kauli yake ikionyesha nia ya kuvishawishi vyama hivyo kuvunjwa.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye ndiye Naibu Kiongozi wa UDA, alirejelea kauli yake kwamba serikali ya Kenya Kwanza imebuniwa kwa mfumo wa kampuni yenye hisa.

Akihutubu katika mkutano huo, Bw Gachagua alisisitiza kuwa “wenye hisa kamili katika uongozi wa Rais Ruto ni wanachama wa UDA.”

“Katika uongozi wa Rais Ruto, kuna umiliki wa hisa. Rais Ruto, wenye hisa wa kweli katika uongozi wako ni wale wameketi hapa (wanachama wa UDA). Hata kama msimamo wetu ni kuwa anafaa kuwafanyia kazi Wakenya wote, wale watakaomsaidia ni wale waliomwamini na kumuunga mkono,” akasema Bw Gachagua.

Kulingana na wadadisi wa siasa, huenda kauli hizo zikairejesha UDA kwenye mkosi ulioiandama Jubilee, kwenye juhudi za kujijenga kisiasa ili kuwa chama kikubwa zaidi, wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Baadhi ya viongozi wa vyama tanzu katika Kenya Kwanza wamekuwa wakipinga juhudi za kuvunja vyama hivyo, hali ambayo imekuwa ikizua mivutano ya kichinichi ya kisiasa.

Vyama ambavyo vimejitokeza wazi kupinga hatua hiyo ni Amani National Congress (ANC) kinachohusishwa na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Ford-Kenya, kinachoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Moses Wetang’ula.

Vyama vingine tanzu ni: Economic Freedom Party (EFP), The Service Party (TSP), Umoja Maendeleo Party (UMP), Tujibebe Wakenya Party kati ya vingine.

Kiujumla, muungano huo una vyama tanzu 18.

Wadadisi wanasema shinikizo la Rais Ruto na Bw Gachagua kwamba lazima vyama hivyo vivunjwe, inarejesha taswira iliyokuwepo katika Jubilee kati ya 2018 na 2022, ambapo viongozi wote walioonekana kuwa waasi au wandani wa karibu wa Rais Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais) walifurushwa.

Baadhi ya wale waliopoteza nyadhifa zao ni Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen kama Kiongozi wa Wengi kwenye Seneti, Gavana wa Nakuru Susan Kihika kama Kiranja wa Wachache katika Seneti, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kama Naibu Spika wa Seneti, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah kama mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge kati ya wengine.

Chama hicho pia kiliwafurusha Maseneta Maalum sita kwa sababu tuhuma za “uasi”, ijapokuwa uamuzi huo ukafutiliwa mbali na mahakama.

Kulingana na mdadisi wa siasa Mark Bichachi, huenda mwelekeo huo ukazua uasi katika UDA na kuvuruga mikakati yake kama ile ya Jubilee.

“Shinikizo wanazotoa viongozi wa UDA kwamba lazima vyama tanzu katika Kenya Kwanza vivunjwe ni hatari sana. Chama kama Ford-Kenya kina historia ndefu ya kisiasa. ANC nacho ni miongoni mwa vyama vyenye ushawishi mkubwa katika eneo la Magharibi. Hivyo, misukumo ya vyama hivyo kuvunjwa ni hatari sana. Inaweza kugeuka mwiba wa kujidunga kwa Rais Ruto na washirika wake,” akasema Bw Bichachi.

Mdadisi huyo alisema kuwa lazima Rais Ruto atahadhari anapotoa msukumo huo, kwani yeye binafsi alikuwa miongoni mwa waathiriwa wakuu wa matukio yaliyoshuhudiwa katika Jubilee.

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Kushiriki tendo la ndoa bila vijisababu...

Hatimaye Wapokomo wapata toleo la Biblia kwa lugha yao

T L