• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
BAHARI YA MAPENZI: Kushiriki tendo la ndoa bila vijisababu huboresha uhusiano

BAHARI YA MAPENZI: Kushiriki tendo la ndoa bila vijisababu huboresha uhusiano

NA BENSON MATHEKA

IKIWA una mazoea ya kufika nyumbani ukiwa umechelewa na kutoa visingizio vya hapa na pale ili kumnyima mume au mke wako haki yake ya tendo la ndoa, unakosea pakubwa.

Unamfanya mumeo au mkeo kushuku uaminifu wako kwa ndoa yenu na haya sio makosa yake, ni yako.

Mtu akianza kumnyima mume au mke wake tendo la ndoa bila sababu maalumu, anavuruga ndoa yake.

Anayefanya hivyo huwa anaweza kumtia mwenzake katika majaribu pia. Watu walio na tabia hii huwa wanasingizia uchovu ili kuwanyima waume au wake wao tendo la ndoa.

Ukweli wa mambo ndio huu; kubadilika ghafla na kuanza kumpimia mchumba wako tendo la ndoa kunaweza kufanya uhusiano wenu kuwa baridi. Hali kama hii inaweza kusuluhishwa kupitia mazungumzo ya wazi katika mazingira ya kuheshimiana.

Ni muhimu kuwasiliana na mume au mkeo ukichelewa kazini ili ajue ulipo badala ya kunyamaza na kufika nyumbani na kisha kutoa visingizio vya hapa na pale kwa kutomtimizia haki yake ya ndoa.

Ikiwa anayelaumiwa anakataa kufanikisha mawasiliano kama vile kutochukua simu au kukataa mazungumzo, huwa anampa mwenzake sababu za kuamini ana mipango ya kando.

Kuna tabia ambazo walio na mipango ya kando huwa nazo kama vile kutowachangamkia wachumba wao wakati wa tendo la ndoa. Hii huwa inasambaratisha uhusiano au kuufanya baridi kiasi cha kukosesha mtu raha ya ndoa.

Unapomnyima mumeo au mke muda wa kuwa naye kwa kuchelewa asikojua huwa unampimia na kumnyima raha ya ndoa. Ni makosa kwa kuwa mtu hafai kumpimia au kumnyima mume au mkewe tendo la ndoa ikiwa hali inaruhusu.

Unafaa kujimwaga mzima mzima kwa mtu wako. Mpe haki yake. Mke akitaka mpe, mume akitaka mchangamkie wakati wowote. Hii itaimarisha raha katika ndoa. Ukianza vijisababu vya kumnyima muda na tendo la ndoa, utachoma ndoa.

Mtu anapoanza kumpimia au kumnyima mwenzake tendo la ndoa bila sababu maalumu huwa anatelekeza jukumu lake.

Tendo la ndoa ni haki muhimu inayounganisha wanandoa. Hivyo basi, mtu akianza kumnyima mwenzake au kumpimia bila sababu maalumu, huwa anavunja ile nguzo ya ndoa.

Hivyo basi, mtu anafaa kutoa mwili wake bila vikwazo kwa mke au mume wake. Ingawa kuanza kuchelewa kufika nyumbani, kutochangamkia ngoma chumbani na kutotaka kuwasiliana na mchumba wako huwa ni ishara mtu ana mipango ya kando, ni muhimu kuthibitisha kwanza.

Inaweza kuwa mtu wako anasema ukweli akikuambia amechelewa kazini au amechoka. Lakini hii haiwezi kuwa kila wakati au kwa siku fulani.

Ikianza kuwa mazoea, basi una sababu ya kushuku lakini muhimu ni kuthibitisha.

Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kuwa kupimia mchumba wako muda na tendo la ndoa sio tu kukiuka viapo vya ndoa bali pia ni kumtia katika majaribu.

Mwandalie mtu wako burudani, mtimizie haki yake ya ndoa, mchangamshe ahisi raha naye hatakushuku.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yasema bado inaweka pamoja ushahidi wa kushtaki...

UDA yaanza kuiga makosa ya Jubilee

T L