• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 4:32 PM
UDA yakataa madai kuhusu ugavi wa mamlaka

UDA yakataa madai kuhusu ugavi wa mamlaka

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimekana ripoti kuhusu uwepo wa mpango wa ugavi wa nyadhifa kati yake na vyama vya ANC na Ford Kenya Naibu Rais akiibuka mshindi na kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kupitia taarifa Jumamosi, Januari 29, 2022, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alisema ripoti hizo ni za uwongo na zilizobuniwa na vyombo vya habari.

Alisisitiza kuwa muungano kati ya UDA, ANC na Ford Kenya unalenga kuwaleta Wakenya pamoja, kupiga jeki uchumi wa nchi na wala sio kufanikisha ugavi wa nyadhifa zozote serikalini.

“Maelezo kuhusu ushirikiano kati ya UDA, na vyama vya ANC, Ford Kenya na vyama vinginevyo ikiwa yatakuwepo, yatatangazwa na vinara wa vyama hivyo wakati mwafaka,” Bi Maina akasema.

Akaongeza: “Kwa hivyo, ningependa kutoa wito kwa wananchi na wafuasi wa vyama hivi kupuuzilia mbali habari kama hizo za uwongo kwani zinalenga kuwapotosha na kusababisha uhasama miongoni mwa vinara katika muungano huo.”

Chama cha UDA kilitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti moja la Jumamosi Januari 29, 2022, kuchapisha habari zilizodai kuwa muungano wa vyama hivyo vitatu, maarufu kama Kenye Kwanza vimeratibu mipango ya ugavi wa mamlaka ikiwa vitashinda na kuunda serikali.

Kulingana ripoti hizo, Bw Mudavadi atateuliwa Mkuu wa Mawaziri na kupewa usimamizi wa Wizara za Fedha na Ugatuzi. Chama chake cha ANC pia kutatengewa nafasi zingine kando na kutoa wagombeaji wa ugavana katika kaunti za Nairobi, Kakamega na Bungoma.

Kwa upande wake, Wetang’ula atatengewa nafasi mbili za uwaziri na kuachiwa nafasi ya kuwasilisha wagombeaji katika kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

Naibu Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa tofauti kati ya UDA na mrengo wa Azimio la Umoja ni kuhusu suala hilo la ugavi wa nyadhifa serikali.

“Sisi tunalenga kuunda serikali ya walala hoi ilhali haja kubwa ya wale tunaoshindana nao ni kuunda vyeo zaidi ili vigawanywe miongoni mwao na wadozi wengine. Hili ndilo lilikuwa lengo lao katika BBI na reggae ambayo ilizimwa na mahakama,” akasema Januari 13, 2022 alipokuwa akisaka kura katika eneobunge la Kwanza, Trans Nzoia.

You can share this post!

Selina wa vishale anatamba kote nchini

Leads United yataka taji la Koth Biro

T L