• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Ugavana: Kesi tatu za Sonko kusikilizwa pamoja

Ugavana: Kesi tatu za Sonko kusikilizwa pamoja

NA RICHARD MUNGUTI

WAPIGAKURA wawili wamepinga uidhinishwaji wa Bi Wavinya Ndeti kuwania Ugavana kaunti ya Machakos huku aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko na chama cha Wiper wakihoji hatua ya IEBC kumnyima fursa ya kuwania Ugavana Mombasa.

Jopo linalosikiliza malalamishi ya Sonko ya kunyimwa uteuzi kuwania Ugavana Mombasa liliamuru kesi tatu zinazopinga uamuzi wa afisa msimamizi wa uchaguzi kaunti ya Mombasa (CRO) Bi Swalha Ibrahim Yusuf ziunganishwe ili kusikilizwa pamoja.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyeandamana na Sonko alisema IEBC imemdhulumu mwaniaji huyu maarufu kwa kuwasaidia wanyonge katika jamii.

“Kesi zote tatu zinazopinga uamuzi wa CRO Bi Yusuf kutomwidhinisha Sonko ziunganishwe zisikilizwe pamoja. IEBC imekubaliwa kujibu madai yaliyoibuliwa na Sonko na Wiper,” jopo linaloongozwa na Bw Wambua Kilonzo liliamuru.

Mawakili Eunie Lumallas na Wilfred Nyamu wanaowakilisha Wiper na Sonko walieleza jopo hilo kwamba kesi ya Sonko iko na changamoto nyingi kwa vile kuna kesi inayopinga uamuzi wa Bunge la Seneti kwa kumtimua kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Lakini jopo hilo liliwaambia mawakili hao wahoji tu “makosa ya CRO peke yake na wala sio midahalo mirefu ya masuala ya kisheria.”

Wiper kinadai IEBC ilikandamiza haki za Sonko na wakazi wa Mombasa kuchagua mwaniaji wanayemtaka.

Na wakati huo huo afisa msimamizi wa uchaguzi eneo la Kisauni Mombasa Bw Ibrahim Wario ameagizwa atafute katika sajili ya wapiga kura jina la mwaniaji kiti Udiwani Wadi ya Junda Bi Lilian Sidi kama lipo.

Ijapokuwa Bi Sidi aliidhinishwa kuwania kiti cha Wadi ya Junda kwa tiki ya Chama cha Kanu hakukabidhiwa cheti kwa vile jina lake halikuonekana katika Sajili ya wapiga kura Kisauni.

Akitoa ushahidi Bi Sidi alieleza jopo la IEBC linalosuluhisha mizozo ya uteuzi (DRC) kwamba alipiga kura 2017 na jina lake lilikuwa katika Sajili lakini halikuonekana katika mtambo wa kieletronik ulio na majina ya wapiga kura.

“Jina langu lilikuwa katika sajili ya 2017 lakini halikuonekana Aprili 20 2022 nilipoidhinishwa na KANU kuwania Udiwani Wadi ya Junda,” Bi Sidi aliambia jopo la DRC linaloongozwa na Bw Wambua Kilonzo.

Bw Wario alipewa muda hadi leo alasiri kutathmini ikiwa jina la Bi Sidi lipo katika sajili ya Kisauni au la.

Katika kesi ya yakupinga uidhishaji wa Bi Ndeti, Mabw Gideon Ngewa Kenya na Kisilu Mutisya waliomba waruhusiwe kumhoji mwaniaji huyo jinsi alivyopata digirii mbili za Uzamili kabla ya kabla ya kuhitimu na digirii ya kwanza.

Bi Ndeti alihitimu katika chuo kikuu cha City University, London,Uingereza na digirii ya Uzamili katika Masuala ya Kompyuta.

Na wakati huo mwaniaji kiti cha Urais Jimmi Wanjigi amewasilisha kesi kupinga uamuzi wa mwenyekiti wa IEBC kumnyima fursa ya kuwania urais kwa madai hana cheti cha digrii.

Kesi itasikilizwa Juni 16, 2022.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Ushuru mpya wa mayai watishia uhusiano wa...

Wanasiasa Mombasa waahidi kufanya kampeni kwa amani

T L