• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
NJENJE: Ushuru mpya wa mayai watishia uhusiano wa kibiashara Kenya na Uganda

NJENJE: Ushuru mpya wa mayai watishia uhusiano wa kibiashara Kenya na Uganda

NA WANDERI KAMAU

HUENDA Kenya na Uganda zikaanza mvutano mpya wa kibiashara, baada ya Kenya kuanza kutoza ushuru mayai yanayoingizwa nchini kutoka mataifa ya nje.

Uganda inasema kuwa Kenya sasa inatoza mayai yake ushuru wa Sh72 kwa trei moja, hatua inayorejesha tena ada iliyokuwa imesimamishwa Desemba iliyopita, baada ya mataifa hayo mawili kufanya mazungumzo.

Wafanyabiashara wa Uganda wamelalamikia vikali hatua hiyo, wakisema haionyeshi nia njema kwenye uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

“Hatua ya Kenya kutoza ada mayai kutoka Uganda haifai hata kidogo. Inaathiri uhusiano wa kibiashara uliopo. Ni hatua inayokiuka sera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu usafirishaji wa bidhaa na huduma bila vikwazo vyovyote miongoni mwa nchi wanachama,” akasema mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Bidhaa Nje nchini Uganda (UNCBT), Bw Godfrey Oundo.

Hata hivvyo, Katibu wa Ufugaji, Harry Kimtai, alisema kuwa ada hiyo ni ushuru wa kawaida ambao hutozwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka mataifa ya nje.

“Sina maelezo ya kina kuhusu ada hiyo japo huenda ikawa malipo ya kawaida ambayo hutozwa bidhaa zinazoagizwa nje na Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA),” akasema.

Mzozo huo mpya unajiri wakati mataifa hayo mawili bado hayajasuluhisha tofauti zake kuhusu maziwa. Hii ni baada ya Kenya kupiga marufuku uingizaji wa maziwa kutoka Uganda mnamo 2019.

Kwa miaka miwili iliyopita, Kenya imekuwa ikidhibiti vikali uingizaji wa mayai na maziwa kutoka Uganda, hali ambayo imeathiri sana mahusiano kati ya nchi hizo mbili. Mvutano kuhusu biashara ya mayai ulisuluhishwa kwa muda baada ya Uganda kutishia kuizuia Kenya kuuza bidhaa zake nchini humo.

Novemba 2021, Baraza la Mawaziri la Uganda liliiagiza Wizara ya Kilimo nchini humo kubaini bidhaa kutoka Kenya ambazo zitapigwa marufuku dhidi ya kuuzwa huko.

Hilo lilionekana kama “ulipizaji kisasi” dhidi ya Kenya kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya bidhaa zake za kilimo.

Mataifa hayo mawili yamekuwa yakivutana mara kwa mara kuhusu masuala ya kibiashara. Mzozo wa sasa ulianza mwaka 2019, baada ya Kenya kuacha kuagiza maziwa aina ya ‘Lato’ kutoka Uganda.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ahadi ya mabwawa Nanyuki imekuwa ni ndoto...

Ugavana: Kesi tatu za Sonko kusikilizwa pamoja

T L