• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Uhuru agawa kazi za Ruto

Uhuru agawa kazi za Ruto

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto ameachwa bila kazi ya kufanya baada ya Rais Uhuru Kenyatta kugawa majukumu yake kwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Hii imefanya Dkt Ruto kujitafutia mambo ya kufanya kama vile harambee makanisani na kuhudhuria sherehe za kufuzu katika vyuo vya kadri.

Hatua hii ni baada ya Rais Kenyatta kumchukua Dkt Matiang’i kuwa msaidizi wake mkuu, jukumu ambalo kikatiba ni la Dkt Ruto.

Kulingana na Katiba, Naibu Rais ndiye msaidizi mkuu wa Rais, na anapaswa kumsaidia kutekeleza majukumu yake.

Rais amekuwa akimtuma Dkt Matiang’i hata katika mataifa ya kigeni licha ya kuwa wizara yake inahusika na usalama wa ndani.

Kiutawala waziri anajikita katika kazi za wizara yake, na ni Rais ama Naibu Rais pekee wanaoweza kuingilia majukumu ya wizara hizo.

Tukio la juzi ni hatua ya Rais Kenyatta kumtuma Dkt Matiang’i nchini Somalia mnamo Jumapili kufikisha ujumbe kwa Rais Mohamed Farmajo, kutokana na mzozo wa kidiplomasia uliopo kati ya mataifa haya mawili.

Na mnamo Jumanne, Dkt Matiang’i alitumwa na Rais Kenyatta nchini Ethiopia kukutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed, kumrai kuisaidia Kenya kusuluhisha tofauti zake na Somalia.

Hii ni licha ya kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Raychelle Omamo angepeleka jumbe hizo, ama rais angemtuma Dkt Ruto kama msaidizi wake mkuu.

Rais alianza kuhamisha kazi za Dkt Ruto kwa Dkt Matiang’i mwaka uliopita kupitia tangazo maalum ambapo alimkweza kusimamia mawaziri wenzake hasa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kabla ya hatua hiyo Dkt Ruto ndiye aliyekuwa akitekeleza wajibu huo.

Baada ya kifo cha Mzee Daniel Moi Februari, Rais Kenyatta akiwa Marekani, alikabidhi jukumu la kuongoza mipango ya mazishi kwa Dkt Matiang’i na kumuacha Dkt Ruto bila wajibu wa kutekeleza.

Kulingana na wadadisi wa siasa, hatua ya kumpokonya Dkt Ruto majukumu umeacha Afisi ya Naibu Rais ikiwa “kivuli tu.”

Wanataja hayo kuwa ishara za wazi kuwa Rais hamwamini tena naibu wake.

“Ni dhahiri kuwa uhusiano kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto umeharibika. Ni nadra Ruto kutengewa majukumu muhimu nchini na nje. Afisi yake inaonekana kushindwa kimajukumu na ile ya Dkt Matiang’i,” alieleza Prof Peter Kagwanja, ambaye ni mchanganuzi wa siasa kwenye mahojiano na Taifa Leo jana.

“Uhusiano huo mbaya umechagiwa na hatua ya Ruto kupinga handisheki na BBI. Wawili hao pia wametofautiana kuhusu vita dhidi ya ufisadi,” aliongeza Prof Kagwanja.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta amemwamini zaidi Bw Odinga kuliko Dkt Ruto, ishara kuu ikiwa ni kumuachia jukumu la kusukuma BBI.

Mnamo Jumanne, Rais Kenyatta alikutana na magavana tisa kutoka Rift Vallet katika Ikulu ya Nairobi kujadili maandalizi ya mkutano wa BBI unaopangwa kufanyika Nakuru hapo Machi 21.

Kwenye mkutano huo, Rais aliwaambia magavana hao kuwa amemwachia Bw Odinga kusimamia mchakato wa BBI.

Hii ni licha ya mkutano huo kuwa katika ngome ya kisiasa ya Dkt Ruto.

Bw Odinga pia amekuwa akitoa maagizo kwa niaba ya Rais Kenyatta.

Kwenye mkutano wa BBI mjini Garissa mwezi uliopita, alisema kuwa amezungumza na Rais Kenyatta kuhusu mgogoro wa elimu unaolikumba eneo hilo, akiahidi suluhisho za haraka.

Pia amekuwa akipokea jumbe mbalimbali kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu serikalini wakiwemo mawaziri kumweleza kuhusu hali ya utenda kazi katika wizara zao.

You can share this post!

Balala lawamani kuhusu makavazi

Lampard asifu mmiliki wa Chelsea kuimarisha klabu

adminleo