• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Uhuru amtuliza Kalonzo

Uhuru amtuliza Kalonzo

Na CHARLESĀ WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka Ijumaa jioni alitembelewa na Rais Uhuru Kenyatta nyumbani kwake Karen, Nairobi.

Kwenye ujumbe alioweka katika akaunti yake ya Twitter Jumamosi alitangaza Bw Musyoka alielezea fahari ya kutembelewa na Rais Kenyatta.

“Ilikuwa ni furaha yangu kumkaribisha nyumbani kwangu Nairobi Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Muigai Kenyatta na kinara mwenzangu katika OKA Seneta wa Baringo Gideon Moi.

“Tuko ndani ya muungano wa Azimio-One Kenya na tutamuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa urais katika uchaguzi mkuu ujao, Agosti 9, mwaka huu,” Bw Musyoka akaongeza.

Rais Kenyatta amemtembelea Kalonzo wiki moja baada ya kigogo huyo wa siasa za Ukambani kuweka kando mipango yake ya kuwania urais mwaka huu na badala yake kutangaza kuwa anamuunga mkono Bw Odinga chini ya mwavuli wa vuguvugu la Azimio la Umoja.

Bw Musyoka alisema alifikia uamuzi huo baada ya kushauriana na viongozi wa chama chake na wafuasi wake.

“Kujiunga na Azimio hakukuwa uamuzi wangu kama mtu binafsi. Watu walitoa maoni na mapendekezo yao na ikaamuliwa kwamba tujiunge na muungano wenye miguu mitatu, Jubilee, ODM na OKA,” akasema.

Hata hivyo, inaaminika kuwa Bw Musyoka alifikia uamuzi huo kutokana na ushawishi kutoka kwa Rais Kenyatta. Aidha, inadaiwa alifanya hivyo kwa misingi ya presha kutoka kwa magavana watatu kutoka Ukambani; Alfred Mutua (Machakos), Profesa Kivutha Kibwana (Makueni) na Bi Charity Ngilu wa Kitui.

Hata hivyo, baada ya kutoa tangazo hilo mnamo Machi 12, 2022, Bw Musyoka amekuwa akitoa kauli za kukanganya.

Wakati mmoja alidokeza kuwa atajiondoa kutoka muungano huo ikiwa Bw Odinga hatamteuwa kuwa naibu wake na kumtengea thuluthi moja ya nyadhifa serikalini.

Na kwenye mahojiano na redio ya Musyi FM mnamo Ijumaa Bw Musyoka alisema haamini kuwa Bw Odinga atatimiza yale yaliyoko mwenye makubaliano ambayo alitia saini katika KICC, Nairobi.

Wakati mmoja alidai Katibu Mkuu wa Wiper Shakila Mohamed hakufahamu yale ambayo yalikuwa katika mkataba alioutia saini pamoja na makatibu wa vyama vingine tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja.

Lakini kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Ijumaa usiku, Bw Musyoka tena alibadili kauli na kusema kuwa yenye na Bi Shakila walifahamu fika masuala yote yaliyokuwa ndani ya mkataba huo.

Wadadisi wanasema ni kutokana na hatua yake ya kutoa kauli za kukanganya imani yake kwa Azimio la Umoja ambapo Rais Kenyatta aliamua kumtembelea kwa mazungumzo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Amri wakili Ojienda alipwe Sh88m

Kadu-Asili yapata pigo kiongozi wake akihamia PAA

T L