• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Uhuru kuwa kocha mkuu wa ‘Team Raila’

Uhuru kuwa kocha mkuu wa ‘Team Raila’

ONYANGO K’ONYANGO na JUSTUS OCHIENG

RAIS Uhuru Kenyatta jana Alhamisi alianza rasmi juhudi za kumsaidia kinara wa ODM Raila Odinga kusaka kura awe mrithi wake atakapostaafu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Rais Kenyatta kwa mara ya kwanza alitangaza kuwa yuko ndani ya muungano wa Azimio la Umoja utakaotumiwa na Bw Odinga kuwania urais.

Katika hafla Ikulu ya Nairobi ambapo wabunge na maseneta wanaounga mkono Azimio la Umoja walihudhuria, Rais Kenyatta alifichua wazi kwamba roho yake iko ndani ya muungano huo.

Kulingana na duru, Rais Kenyatta alikutana faraghani na Bw Odinga pamoja na viongozi wa Wengi na Wachache kwenye Bunge la Kitaifa na Seneti, ambapo alitangaza msimamo wake.

Kiongozi wa nchi aliwahimiza maseneta kupitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa 2021 kabla ya mwezi ujao, kama njia ya kumnyooshea Bw Odinga njia ya kuelekea Ikulu.

Iwapo Mswada huo utapitishwa, Bw Odinga atawania urais kupitia tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja badala ya ODM.

“Rais Kenyatta alitumia mfano wa mechi ya soka ambapo alisema kuwa Bw Odinga atakuwa kapteni na yeye atakuwa kocha kuhakikisha kuwa muungano wa Azimio la Umoja unashinda Uchaguzi Mkuu ujao,” mmoja wa viongozi waliohudhuria mkutano huo wa faragha aliambia Taifa Leo.

Rais Kenyatta ameshikilia kuwa atajihusisha na siasa za Uchaguzi Mkuu ujao katika juhudi za kusaka mrithi wake, ambapo amejitokeza wazi kuonysha chaguo lake ni Bw Odinga.

KIBARAKA

Kauli hiyo imekuwa ikimkasirisha Naibu Rais William Ruto, ambaye anasema kinara wa ODM atakuwa kibaraka cha mabwanyenye iwapo atachaguliwa kuwa rais.

“Tunawaambia watu wanaotaka Kenya kuwa na rais ‘atakayekanyaga’ Bunge na Idara ya Mahakama kuwa Wakenya hawako tayari,” akasema Dkt Ruto aliyekuwa akizungumza Alhamisi alipokuwa akihutubia msururu wa mikutano ya kisiasa mtaani Eastlands jijini Nairobi.

Jumamosi, Bw Odinga atazindua kampeni zake za urais mjini Thika, Kaunti ya Kiambu, ambayo ni ngome ya Rais Kenyatta.

Jana Alhamisi, Rais Kenyatta alionekana kuwapa mwelekeo wandani wake kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakimshutumu kwa kusalia kimya bila kuwaonyesha ‘njia’.

Baadhi ya wabunge na maseneta wa vyama vilivyo katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA) unaojumuisha Mabw Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Cyrus Jirongo (UDP) walihudhuria kikao hicho cha Ikulu, Alhamisi.

Bw Mudavadi jana Alhamisi aliambia Taifa Leo kuwa hakupokea mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo.

“Sikualikwa na kuna uwezekano kwamba wabunge wa chama changu walialikwa. Siwezi kuzungumzia mkutano ambao sijui ajenda yake,” akasema Bw Mudavadi.

Rais Kenyatta kwenye dhifa hiyo alisema kuwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ukipitishwa utatoa nafasi kwa vyama vingi kuunda muungano thabiti utakaoibuka na ushindi.

Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, Joshua Kutuny, ambaye pia ni Mbunge wa Cherang’any, alisema kuwa Rais Kenyatta aliwasihi viongozi waliohudhuria hafla hiyo kusalia pamoja kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

  • Tags

You can share this post!

Uchungu wa mama

Kivumbi chanukia Boston Marathon ikivutia Kamworor, Bekele

T L