• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Umaarufu wa UDA kwenye ngome kuu watiliwa shaka

Umaarufu wa UDA kwenye ngome kuu watiliwa shaka

WALTER MENYA NA ONYANGO K’ONYANGO

MCHUJO wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) uliomalizika jana umetikisa Naibu Rais William Ruto huku uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ukikaribia, malalamishi yakizidi na walioshindwa wakihama chama hicho kuwa wagombeaji huru.

Zoezi hilo ambalo Dkt Ruto alisimamia, lilishuhudia idadi ndogo ya wanachama katika ngome zake na kutilia shaka umaarufu ambao chama hicho kimekuwa kikijigamba kinafurahia, hasa eneo la Rift Valley na Mlima Kenya.

Chama hicho kilitarajia kutumia kura za mchujo ya Alhamisi kuonyesha umaarufu wake, haswa katika maeneo ya Rift Valley na Mlima Kenya.

Lakini matokeo ya shughuli hiyo yaliyotangazwa Ijumaa yalionyesha taswira tofauti kwa misingi ya idadi ndogo ya watu waliojitokeza kupiga kura katika jumla ya kaunti 34 nchini.

Japo Dkt Ruto hudai kuwa UDA ina jumla ya wanachama milioni 8, kauli hiyo ni ya kutiliwa shaka kwani ni wanachama wachache mno walijitokeza, haswa katika ngome hizo mbili.

Chama hicho kilichoundwa mwaka jana, hudaiwa kuwa kiliyeyusha ushawishi wa Rais Uhuru Kenyatta na chama tawala, Jubilee katika maeneo ya Mlima Kenya na Rift Valley.

Ithibati kwamba, ni idadi ndogo ya wapiga kura walioshiriki mchujo wa UDA ni katika kaunti ya Kiambu, ambayo mnamo 2017 ilikuwa na jumla ya wapiga kura 1,180,920 Lakini ni wapiga kura 138, 384 walioshiriki katika mchujo wa ugavana kwa tiketi ya chama hicho ambacho ni mshirika mkuu katika muungano wa Kenya Kwanza.

Hii ni tofauti kabisa na kinyang’anyiro sawa na hicho mnamo 2017 ambapo jumla ya wapiga kura 423,520 walishiriki katika mchujo ambapo Ferdinand Waititu aligarazana na William Kabogo kushindania tiketi ya ugavana kwa udhamini wa Jubilee.

Ushahidi mwingine kwamba, kura ya mchujo ya UDA ilivutia idadi ndogo ya wapiga kura ilijitokeza katika kaunti ya Uasin Gishu, anakotoka Dkt Ruto.

Kulingana na takwimu za 2017, jumla ya wapiga kura 209, 550 walishiriki katika kura za mchujo kusaka mgombeaji wa ugavana kwa tiketi ya Jubilee.

Lakini mambo yalikuwa tofauti Alhamisi wiki jana kwa sababu takwimu zinaonyesha kuwa ni wapiga kura 179,970 walishiriki zoezi hilo.

Hii ni licha ya kwamba, chama cha UDA kilitumia sajili ya IEBC badala ya sajili yake iliyoidhinishwa na Afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Ki – siasa.

Hii ina maana kuwa, kuna uwezekano mkubwakwamba, wafuasi wa muungano wa Azimio walishiriki katika zoezi hilo, haswa katika kaunti ya Uasin Gishu yenye mseto wa makabila.

Kulingana na sheria mpya ya Vyama vya Kisiasa, wale walio kwenye sajili ya wanachama wa vyama vya kisiasa ndio wanafaa kushiriki katika kura za mchujo.

Katika kaunti ya Nakuru, uchaguzi huo wa mchujo ambao ulitarajiwa kuibua ushindani mkali ulishuhudia idadi ndogo ya wapiga kura katika maeneo bunge 11.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa ndogo zaidi hivi kwamba, baadhi ya maafisa wa kus – imamia shughuli hiyo waliwashauri washindi kubadili mikakati ikiwa wanatarajia kumwezesha Dkt Ruto kushinda uchaguzi wa urais Agosti 9.

“Inavunja moyo kwamba, idadi ndogo ya wapiga kura wamejitokeza katika eneo hilo linalochukuliwa kuwa ngome ya Naibu Rais. Sharti tujiulize ni kwa nini wafuasi wa UDA walisusia kura hii ya mchujo.

Kwa mfano, katika eneo bunge la Subukia ambalo ni ngome ya UDA, kati ya wapiga kura 81,144 katika sajili ya IEBC ni wafuasi 18, 690 pekee wa UDA walijitokeza kushiriki kura ya mchujo Alhamisi.

Idadi hii inawakilisha asilimia 23 pekee ya jumla ya wapiga, hali ambayo inaitia wasiwasi UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Idadi ndogo ya wafuasi wa UDA pia walijitokeza kwa shughuli hiyo katika kaunti za Murang’a, Nyeri, Embu, Tharaka Nithi, miongoni mwa mingine katika Mlima Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Juventus na Bologna nguvu sawa

Raila atashinda urais kwa asilimia 60 – Peter Kenneth

T L