• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Vigogo Azimio wakunja mkia kuhusu teuzi EALA

Vigogo Azimio wakunja mkia kuhusu teuzi EALA

NA MARY WANGARI

VIGOGO wa Azimio jana Jumatano walilemewa na presha na kulazimika kuondoa jamaa zao wanaomezea viti vya ubunge Afrika Mashariki (EALA).

Bw Jalan’go Midiwo ambaye ni binamu yake kinara wa Azimio, Raila Odinga, na kakake aliyekuwa mbunge wa Gem, Jakoyo Midiwo, mwanawe kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kennedy Musyoka, mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi ni miongoni mwa waliojiondoa katika dakika ya mwisho.

Majina ya dada yake Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta, Bi Christine Pratt, pamoja na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat vilevile hayakuwepo katika orodha iliyowasilishwa na muungano wa Azimio.

Hata hivyo, bintiye Kiongozi wa ODM, Winnie Odinga, ni miongoni mwa wagombea sita walioteuliowa na Azimio kushiriKI mchujo wakiwemo mfanyabiashara maarufu Suleiman Shahbal, Justus Kizito, Timothy Bosire, Mohamed Diriye, na Beatrice Askul.

Hatua ya Bw Moi kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho chenye ushindani mkali ilitangazwa na msemaji wa One Kenya Alliance, Fred Okango.

“Kufuatia maombi yaliyowasilishwa na mheshimiwa Gideon Moi na uteuzi wake kuwa mbunge wa EALA, Moi angependa kushukuru KANU na muungano wa Azimio One Kenya kwa fursa hiyo na kuwa na imani naye. Anawatakia kila la kheri katika juhudi zao,” ilisema taarifa.

Mbunge huyo wa zamani wa Baringo ya Kati alikuwa ametuma maombi ya kugombea wadhifa huo licha ya nyadhifa za wabunge tisa watakaowakilisha Kenya katika EALA kutengewa vyama vikuu vya kisiasa nchini: UDA, ODM, Wiper na Jubilee.

UDA yake Rais William Ruto vilevile iliwasilisha orodha ya majina 15 kuwania ubunge wa EAlA wanaojumuisha aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar, aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Rais Ruto kilichovunjuwa cha URP, na aliyekuwa mbunge mteule David Sankok.

Aliyekuwa mbunge maalum Kaunti ya Nandi Zipporah Kering, Rebecca Lowoiya, Godfrey Maina, Okengo Nyambane, Falhadha Iman, Abdikadir Aden, Jonas Kuko, Kubai Iringo, Lilian Cheptoo, Yasser Bajaber na Salim Mohammed ni miongoni mwa walioteuliwa kushiriki mchujo huo.

Kenya imetengewa nyadhifa tisa za wabunge watakaoiwakilisha katika EALA ambapo kambi ya Kenya Kwanza, ambayo ni Upande wa Wengi itashirikisha wagombea 15 huku Upande wa Wachache (Azimio) ukiwa na 12.

Kenya Kwanza imetengewa nafasi tano za wabunge huku zilizosalia nne zikiendea Azimio.

Azimio inatarajiwa kugawanya nyadhifa hizo nne miongoni mwa vyama vyake tanzu huku ODM ikitengewa vinne, Jubilee na Wiper zikipata nafasi moja moja.

Uchaguzi wa kugombea nyadhifa za ubunge wa EALA utafanyika Novemba 17 wiki chache tu kabla ya hatamu ya bunge la sasa la EALA kukamilika mwezi ujao, Disemba 17, 2022. Ni Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pekee ambazo bado hazijawasilisha majina ya wabunge wake tisa watakaoziwakilisha katika Bunge la Afrika Mashariki.

Sheria za EALA 2011 zinaelekeza kuwa Bunge jipya lichaguliwe katika muda wa siku 90 kabla ya muda wa bunge linalohudumu kukamilika, hivyo kumaanisha kwamba Kenya imechelewa kufanya hivyo.

  • Tags

You can share this post!

Masharti makali ya IMF yanyonga raia

JURGEN NAMBEKA: Vijana wachangamkie miradi wanayoundiwa...

T L