• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
JURGEN NAMBEKA: Vijana wachangamkie miradi wanayoundiwa kujiendeleza

JURGEN NAMBEKA: Vijana wachangamkie miradi wanayoundiwa kujiendeleza

NA JURGEN NAMBEKA

VIJANA wengi eneo la Pwani na sehemu zingine nchini wamefumbia macho fursa ya kujiendeleza kiuchumi na kielimu.

Kutokuwa na habari kuhusu fursa zilizopo mahususi kwa ajili yao, kumewafanya wengi kukata tamaa maishani.

Katika pilkapilka zangu za hapa na pale jijini Mombasa, nilikutana na vijana ambao motisha yao iliwasukuma kutafuta njia mbadala za kujiendeleza, licha ya changamoto haba zilizopo.

Kupitia mitandao ya kijamii walipata mwaliko kutoka Wakfu wa Aga Khan kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU), kujiandikisha kwa mafunzo ya wiki sita mtandaoni kuwainua kiuchumi.

Kati ya vijana waliojiunga na mradi huo, ni 89 pekee walifuzu mwishoni mwa mafunzo hayo yasiyo na malipo.

Wachache hao walipata nafasi ya kuwasilisha mawazo ya kibiashara mbele ya majaji na wawekezaji na kuwapa mwanzo mpya.

Cha kusikitisha ni kuwa, kuna wengi wa vijana kutoka kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu ambao walikufa moyo katikati ya mafunzo na kujiondoa. Ole wao kwani waliostahimili walipata kutuzwa.

Jambo lililojitokeza ni kuwa, hata panapotokea nafasi za kujiendeleza vijana kadhaa wanakosa kuzichangamkia ili wafaidike.

Suala hili si geni kwani kuna wengi tu nchini walipuuza Mradi wa Nafasi za Ajira kwa Vijana (KYEOP), unaolenga vijana walio kati ya miaka 18-35 katika maeneo ya mjini na mashambani, kuwapa mafunzo, fursa za uanagenzi na ufadhili wa kibiashara.

Mafunzo hayo sio ya darasani ila wanaojisajili hupelekwa kwa wataalamu mbalimbali ili kujifunza moja kwa moja kazini.

Kwa mfano, kijana atapelekwa kwa msusi shupavu, seremala, mwashi na kadhalika akapate ujuzi wa taaluma anayotaka.

Kwa vijana wengi niliokutana nao na kujaribu kuwauliza kuhusu miradi kama hiyo ya Agha Khan na KYEOP, walionekana kutojua ipo, tena kwa ajili yao.

Huenda serikali haijafanya juu chini kuwafikishia habari hizo au waliopata habari wana pupa na hawadiriki kula tamu.

Hata hivyo, ni wazi kuwa iwapo vijana nchini – ambao labda masomo yalikatika kwa kukosa namna au walianzisha biashara ikakosa kunawiri kwa kutokuwa na mtaji – wangejua mipango hiyo iliyopo kwa ajili yao, wangefaidi sana.

Nahimiza waandalizi wa miradi hiyo waweke bidi kuhamasisha umma kuyahusu.

Nao vijana wa Pwani na nchi nzima kwa jumla wawe tayari kuzamia nafasi zinazojitokeza bila kukoma, kwani kismati kinaweza kutokea hapo.

Wasipuuze kwa dhana kwamba sio za kweli au zitachukua muda kuzaa matunda.

Wasihofu masharti ili wafaidi, ni vyema wayafuate kikamilifu.

  • Tags

You can share this post!

Vigogo Azimio wakunja mkia kuhusu teuzi EALA

KINYUA KING’ORI: Wandani wa kinara wa Azimio...

T L