• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Ruto awarai vijana kutotumiwa kuzua ghasia

Ruto awarai vijana kutotumiwa kuzua ghasia

SHABAN MAKOKHA na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto mnamo Jumamosi aliwarai vijana kutowaruhusu wanasiasa kuwatumia kuzua ghasia ielekeapo 2022.

Akirejelea tukio ambapo magari kadhaa yaliyokuwa kwenye msafara wake yalirushiwa mawe na vijana wenye ghadhabu katika Kaunti ya Busia, Dkt Ruto aliwaambia wapinzani wake kuangazia juhudi za kubuni ajira kwa vijana badala ya kuwatumia ili kujifaidi.

“Tungetaka kuwaambia wale wanaowatumia watoto wetu kuzua ghasia kwa kuwalipa ili kuwarushia mawe wapinzani wao kwamba siku zao zimehesabiwa. Ikiwa baadhi ya viongozi hawana ajenda, wanapaswa kukoma kutumia mbinu za kisiasa zilizopitwa na wakati kama kuwashinikiza vijana kuwarushia mawe washindani wao,” akasema Dkt Ruto.

Kwenye tukio hilo, msafara wa Dkt Ruto ulikumbana na upinzani mkali ulipojaribu kuingia mjini Busia.

Vijana wenye ghadhabu walijaribu kuuzuia, ijapokuwa hatimaye alifaulu.

Hata hivyo, magari manne yaliyokuwa kwenye msafara huo yaliharibiwa vibaya baada ya kurushiwa mawe na vijana hao.

Licha ya kizaazaa hicho, Dkt Ruto alifanikiwa kuhutubia mkutano mjini humo, baada ya polisi wa kukabiliana na ghasia kuingilia kati na kuwatawanya.

Mbunge Didmus Barasa (Kimilili) alilazimika kupelekwa katika mahali salama na wasaidizi wake, kutokana na ghasia hizo.

Kwenye mkutano huo, Dkt Ruto alisisitiza kuhusu haja ya vijana kuwachagua viongozi watakaowasaidia kutatua changamoto zao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tatizo kuu linalowakumba vijana leo ni ukosefu wa ajira. Hiyo ndiyo sababu ambapo wanapaswa kuwachagua viongozi watakaowasaidia kutatua changamoto zao,” akasema.

Dkt Ruto pia alihutubu katika maeneo ya Bumala, Nambale, Adungosi na Malaba.

Kando na Bw Barasa, viongozi wengine waliokuwa pamoja naye ni wabunge Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Aden Duale (Garissa Mjini) na aliyekuwa mbunge wa kaunti hiyo, Mary Emase.

Tukio hilo linajiri baada msafara wake kushambuliwa tena na vijana wenye ghadhabu katika eneo la Naro Moru, Kaunti ya Nyeri mwezi Septemba.

Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) imekuwa ikiwaonya wanasiasa dhidi ya kuwatumia wafuasi wao kuzua ghasia.

You can share this post!

Dortmund yakung’uta Arminia na kukaribia Bayern...

Mount afunga mabao matatu na kuongoza Chelsea kukomoa...

T L