• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Viongozi wa OKA wataka Moi ataliki Uhuru ajiunge na muungano wao

Viongozi wa OKA wataka Moi ataliki Uhuru ajiunge na muungano wao

Na SAMWEL OWINO

VIONGOZI wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wamemtaka kinara wa Kanu, Seneta Gideon Moi kutalikiana na Rais Uhuru Kenyatta kwa kuvunja ushirikiano na chama cha Jubilee.

Msimamo wa kisiasa wa Seneta huyo wa Baringo, ni miongoni mwa ajenda kuu zilizojadiliwa jana na viongozi wenzake wa OKA; Moses Wetang’ula (Ford Kenya), Musalia Mudavadi (ANC) na Kalonzo Musyoka (Wiper) walipokutana mtaani Karen, Nairobi.

Baada ya mkutano huo, watatu hao walitangaza kuvunjwa kwa muungano wa NASA uliobuniwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa mwaniaji wake wa urais.

Vyama vya ANC, Wiper na Ford Kenya jana vilimwandikia rasmi Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu kumfahamisha kuwa vimejiondoa katika NASA.

Mmoja wa viongozi waliohudhuria mkutano wa jana, aliambia Taifa Leo kuwa Bw Moi ameongezewa muda wa kuvunja mkataba wa maelewano baina ya Kanu na Jubilee.

Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat, wiki iliyopita, alisema kuwa chama hicho kikongwe hakiko tayari kujiunga na OKA kwani kingali na mkataba wa ushirikiano na Jubilee.

Jana, Mabw Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula walisema kuwa talaka ya Bw Moi na Rais Kenyatta itawawezesha kusajili muungano wao wa OKA.

Bw Moi anaonekana kuegemea upande wa Bw Odinga ambaye ameonyesha dalili za kuwania urais 2022.Mwenyekiti wa Kanu hakuhudhuria mkutano wa jana wa vinara wa OKA.

Bw Musalia alisema kuwa mkutano huo ulikuwa wa vinara wa NASA hivyo kiongozi wa Kanu hakutakiwa kuwepo.

“Mkutamo huu ulikuwa wa viongozi wa vyama vilivyo chini ya NASA, Bw Moi anafahamu kinachoendelea hapa. Hivyo, hakuna haja ya kuuliza kwa nini hayuko hapa,” akasema Bw Mudavadi.

Katika mkutano wa jana, viongozi hao waliafikiana kuwa wataendelea na mipango ya kusajili rasmi muungano wa OKA. Chama cha Kanu kitaruhusiwa tu kujiunga na muungano huo iwapo utatamatisha ushirikiano wake na chama tawala cha Jubilee.

Kikosi maalumu kinaendelea na shughuli ya kuandaa manifesto ya OKA katika hoteli ya Manzoni na kinafaa kuwasilisha ripoti yake ya awali kwa viongozi wa OKA kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu alisema kuwa Bw Moi anafaa kufuata nyayo za viongozi wenzake kwa kuvunja mkataba na Jubilee.

“Sasa tutasajili OKA kuwa muungano rasmi kwa sababu tumejiondoa NASA. Tukimaliza kufanya mikakati, tutafungua milango kwa vyama vingine, ikiwemo Kanu,” akasema Bw Mulu.

Kulingana na sheria, chama hakifai kujiunga na zaidi ya muungano mmoja. Hiyo inamaanisha kuwa chama cha Kanu hakina budi kuvunja mkataba wake na Jubilee uliotiwa saini mara baada ya uchaguzi wa 2017.

Lakini Bw Salat anasema Kanu haijakosana na Jubilee hivyo hakuna sababu ya kuvunja mkataba.

“Sijawahi kuona muungano ambapo watu wanapewa masharti. Hawakutueleza walipojiunga na NASA hivyo hatuwezi kufuata upepo kwa kutaliki Jubilee,” akasema Bw Salat.

You can share this post!

Rais Suluhu, SADC waomboleza kifo cha waziri wa ulinzi wa TZ

Serikali yatoa Sh17.4 bilioni kufadhili masomo katika shule...