• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wabunge 12 wajaribu kuvunja laana ya kura

Wabunge 12 wajaribu kuvunja laana ya kura

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE 12 wanakabiliwa na hatari ya kupoteza katika uchaguzi wa Agosti 9 ikiwa wapiga kura wa maeneo yao wataendeleza mtindo wa kutochagua mbunge kwa zaidi ya kipindiu kimoja.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa tangu 1997, wakazi wa maeneo bunge 12 wamekuwa wakiwatema wabunge wao na kuwachagua wapya kila baada ya miaka mitano.

Maeneo bunge hayo ni Kiharu, linalowakilishwa na Ndindi Nyoro, Tetu (James Gichuhi Mwangi), Rangwe (Dkt Lilian Gogo), Alego Usonga (Samuel Atandi), Kilifi Kusini (Ken Chonga), Kaloleni (Paul Katana), Mbooni (Erustu Kivasu) na Kangundo (Fabian Kyule).

Maeneo bunge mengine ni Molo linalowakilishwa na Francis Kuria Kimani, Butula (Joseph Maero Oyula), Mugirango Kaskazini (Joash Nyamoko Nyamache) na Kasarani (Mercy Gakuya).

Wachanganuzi wa siasa na uongozi wanasema baadhi ya sababu zinazochangia wabunge wengi kutemwa baada ya kuhudumu muhula mmoja pekee ni kuwapuuza wakazi na kukosa kutimiza ahadi walizotoa nyakati za kampeni.

“Sababu kuu ya wabunge kutemwa huwa ni utendakazi mbaya na kutoonekana wakitetea masilahi wa wakazi wa maeneo yao nje na ndani ya bunge. Hii ndio maana wapiga kura katika maeneo bunge haya 12 huchagua wabunge wapya kila baada ya miaka mitano wakijaribu kusaka kiongozi atakayewafaa kimaendeleo na kiuwakilishi,” anasema Bw Barasa Nyukuri.

Hata hivyo, anaonya kuwa mwenendo huo wa wapiga kura kubadilisha wabunge kila baada ya miaka mitano hulemaza maedeleo katika maeneo bunge husika.

“Hii ni kwa sababu wanasiasa wana tabia ya kupuuza miradi ya maendeleo iliyoanzisha na watangulizi wao. Wao huanzisha miradi mipya ili kuacha kumbukumbu na kujijengea sifa kwa manufaa yao ya kisiasa” Bw Nyukuri anaeleza.

Lakini Bw Nyoro, ambaye anatetea kiti chake kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) ameapa kuvunja mkosi wa kutochaguliwa kwa mara ya pili kwa wabunge wa Kiharu tangu 1992.

Kulingana na sajili rasmi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), jumla ya wagombea 2,098 wamejitosa ulingoni kung’ang’ania kuwakilisha maeneo bunge 290 nchini huku 385 wakisaka nafasi 47 za wabunge wawakilishi wa kike.

Hii ina maana kuwa jumla ya wagombeaji 1,808 watakosa nafasi ya kuwakilisha mojawapo ya maeneo bunge hayo 290.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya wanunua unga kwa bei ya juu licha ya ahadi ya rais

Zimbabwe yaruhusu biashara ya bidhaa zilizotengenezwa kwa...

T L