• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wabunge wa Tangatanga wasema hawaogopi kupokonywa nafasi zao bungeni

Wabunge wa Tangatanga wasema hawaogopi kupokonywa nafasi zao bungeni

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mrengo wa Tangatanga ambao wanakabiliwa na tisho la kupokonywa nafasi zao katika kamati za bunge la kitaifa, wamesema hawatishwi na hatua hiyo.

Baadhi yao waliosema na Taifa Leo kwa njia ya simu, Jumatano, walisema hawatakoma kumuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto.

“Ndio nimepokea barua ya kunitaka nielezee ni kwa nini nisipokonywe nafasi yangu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kawi. Lakini nawaambis waendelee na mipango yao kwani sitishwi na hatua hiyo,” akasema Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria.

Bw Gikaria alifichua kuwa yeye na wenzake wanalengwa kwa sababu wanaunga azma ya Dkt Ruto ya kuingia ikulu “pamoja na kwamba tulipinga mswada wa vyama vya kisiasa juzi bungeni,”

Naye Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Cate Waruguru alisema hana wasiwasi kwamba Jubilee inapanga kumpokonya wadhifa wake wa naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo.

“Niko tayari kwa lolote lile kutoka kwa chama cha Jubilee ikiwemo kuigura chama cha Jubilee na kujiunga rasmi na chama cha United Democratic Alliance (UDA),” akasema mbunge huyo aliyerejea katika kambi ya Dkt Ruto mnamo Oktoba, mwaka jana.

Mnamo Jumanne chama cha Jubilee kiliwaandikia barua wabunge saba wa mrengo wa tangatanga kilielezea nia ya kuwapokonya nafasi zao za uongozi katika kamati za bunge.

Katika barua ambayo walitumiwa na Kiranja wa Wengi Emmanuel Wangwe, wabunge hao walipewa makataa ya siku sababu wajitetee la sivto wapoteze nafasi hizo.

“Umepewa muda wa siku saba ujitete baada ya chama cha Jubilee kilichokupendekeza kuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu kawi kuamua kukuondoa kutoka wadhifa huo kwa kukiuka misimamo yake ndani na nje ya bunge,” ikasema barua ambayo alitumiwa Bw Gikaria.

Wengine waliotumiwa barua kama hiyo ni; mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Mashauri ya Kigeni Katoo Ole Metito, Kareke Mbiuki (Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira) na William Kisang (Mwenyekiti wa Kamati ya ICT).

Wengine ni; mwenyekiti wa Kamati Utangamano wa Kikanda Ali Wario, Khatibu Mwashetani (naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Ardhi), Gathoni wa Muchomba (naibu mwenyekiti wa kamati ya uchukuzi) na naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Moses Lessonet.

“Ikiwa utatoa majibu ya kuridhisha, suala hilo halitaendelea kupitia barua hii. Ikiwa hakuna maelezo ya kuridhisha yatatolewa, chama kitakuwa huru kuwaondoa kutoka nafasi hizo,” Bw Wangwe akaeleza.

Hii ina maana kuwa wabunge hawa wataondolewa rasmi kutoka nafasi zao katika kamati husika bunge litakaporejelea vikao vyake Januari 25, 2022.

Tulipomfikia kwa njia ya simu, Kiongozi wa wengi Amos Kimunya alisema mabadiliko katika uanachama na uongozi wa kamati za bunge hufanywa kila mara kuimarisha utendakazi.

“Kuteuliwa au kuondolewa kwa wabunge kutoka kamati za bunge kunahusishwa na uungwaji mkono wa ajenda ya kiungozi wa chama,” akasema Bw Kimunya.

Hata hivyo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba hatua hii imechochewa na hatua ya wabunge hao kuungana na wenzao wa kambi ya Dkt Ruto kupinga mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa.

Walifanya hivyo katika vikao maalum vilivyoitishwa kujadili mswada huo mnamo Desemba 29, 2021 na Januari 5, 2022.

Ilisemekana kuwa wabunge ambao hawaungi mkono ajenda ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuunganisha nchi sharti waadhibiwe.

  • Tags

You can share this post!

Wanjigi aachiliwa bila kushtakiwa

Raila acheza karata hatari

T L