• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Wafuasi njiapanda Raila akikana Ruto

Wafuasi njiapanda Raila akikana Ruto

NA CHARLES WASONGA

MIKAKATI ya kisiasa ya kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga inaonekana kuchanganya wafuasi pamoja na wandani wake baada ya kutangaza kutotambua serikali ya Rais William Ruto.

Baadhi yao kama vile aliyekuwa ajenti wake mkuu katika uchaguzi wa urais Agosti 9, 2022, Saitabao Ole Kanchory sasa wanamtaka mwanasiasa huyo mkongwe kuwapa mwelekeo unaoeleweka au atulie.

“Tupe mwelekeo au ufyate. Wakenya hawana wakati wa kuendelea kuzungushwa katika michezo hii isiyo na maana,” akasema Bw Kanchory.

Mnamo Jumatatu, kinara huyo wa Azimio la Umoja-One Kenya alitangaza kuwa muungano huo hautambui uhalali wa Rais William Ruto na maafisa wanaohudumu katika serikali yake ilhali juzi aliwatuma wandani wake kuomba ufadhili wa miradi ya maendeleo kutoka kwa Dkt Ruto.

“Sisi kama Azimio tunapinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hatuwezi kutambua utawala wa Kenya Kwanza na tunaichukulia kama serikali haramu. Hatumtambui William Ruto kama Rais wa Kenya na maafisa wote wanaohudumu chini yake,” Bw Odinga akasema kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo kufuatia ufichuzi uliodai kuwa yeye (Odinga) ndiye alishinda katika uchaguzi wa urais. Kulingana na mfichuzi huyo anayedaiwa kuwa mfanyakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Odinga alipata kura 8,170,353 ikiwa ni sawa na asilimia 57.3 dhidi ya Rais Ruto aliyepata kura 5,915,973 (asilimia 41.66).

Lakini kulingana na matokeo yaliyotangazwa na aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Dkt Ruto alipata kura 7,176, 141 (asilimia 50.46) dhidi ya kura 6,942,930 (asilimia 48.5) za Bw Odinga.

Lakini siku mbili kabla ya Rais Ruto kuanza ziara yake ya siku mbili katika kaunti za Homa Bay, Kisumu na Siaya, Bw Odinga alikutana na viongozi waliochaguliwa kutoka eneo hilo Januari 16 jijini Nairobi na kuwashauri kushirikiana na serikali kuu katika nyanja ya maendeleo.

Wadadisi sasa wanasema hatua ya Bw Odinga kubadili msimamo na kuamua kutotambua uhalali wa serikali ya Rais Ruto sasa imewaacha wafuasi wake katika Luo Nyanza kwenye njia panda.

“Bila shaka sasa wafuasi hao waliotarajia kufaidi kutokana na miradi ya maeneo ambayo Rais Ruto aliahidi kuwa serikali yake itatekeleza katika eneo la Luo Nyanza sasa huenda wakaingiwa na wasiwasi wa kukosa kufaidi,” anasema Profesa Gitile Naituli, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Multi-Media.

Msimamo wa Bw Odinga, pia umeonekana kuwakanganya magavana wa mrengo Azimio ambao majuma mawili yaliyopita waliwapa “idhini” ya kufanya kazi na serikali ya Rais Ruto katika nyanja ya maendeleo.

Duru zasema ni kutokana na kuchanganyikiwa kwa magavana hao ambapo wote 20 walisususia mkutano wa Kamukunji Jumatatu.

Aidha, wabunge wote kutoka eneo la Luo Nyanza hawakuhudhuria mkutano huo, jambo ambalo liliwaacha wengi na maswali mengi bila majibu.

  • Tags

You can share this post!

Ugaidi watishia tena juhudi za kufufua utalii kisiwani Lamu

TAHARIRI: Serikali yafaa irahisishe harakati ya kuingia...

T L