• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wagombeaji huru waungana

Wagombeaji huru waungana

NA WINNIE ATIENO

WAGOMBEA huru takriban 100 wa viti tofauti vya kisiasa katika Kaunti ya Mombasa, wameunda muungano ili kupata nafasi bora ya kushindana dhidi ya wapinzani wanaowania kupitia kwa vyama mbalimbali.

Wakiongozwa na mwenyekiti, Bw Mohamed Amir, ambaye ni kaka mkubwa wa Gavana Hassan Joho, wanasiasa hao waliwashauri wapigakura kutofanya uchaguzi kwa msingi wa vyama bali wachague viongozi wanaoweza kuwaletea mabadiliko.

Kulingana nao, upigaji kura kwa wanasiasa wa chama kimoja, almaarufu kama mfumo wa suti, umechangia uongozi mbaya Mombasa.

“Hiyo ni njia moja ya kuchagua viongozi wazembe,” akasema Bw Amir.

Alidai kuwa, Mombasa haijafaidika kwa kumchagua Seneta Mohammed Faki katika uchaguzi uliopita ilhali Chama cha ODM kimempa tena tikiti kuwania wadhifa huo ifikapo Agosti 9.

Bw Amir, ni mmoja wa wanasiasa waliohama Chama cha United Democratic Alliance (UDA) baada ya kubanduliwa kwenye kura za mchujo Aprili.

Chama hicho kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kilimpa tikiti ya moja kwa moja Bw Hassan Mwaguya, ikasemekana hatua hiyo ilichukuliwa baada ya UDA kufanya kura za maoni zilizoonyesha yeye ndiye alikuwa maarufu kumliko Bw Amir.

Hata hivyo, wanasiasa waliokosa tikiti za UDA katika Kaunti ya Mombasa walidai kuwa wanasiasa wenye umaarufu mkubwa kwenye chama hicho ndio waliobanduliwa nje.

“Tumeamua kugombea nyadhifa mbalimbali za siasa baada ya kunyimwa tikiti kwa sababu ya ushawishi kutoka kwa wafuasi wetu. Lakini kufikia sasa hatujapata kiongozi anayegombania ugavana wala urais ambaye tutamuunga mkono. Tutafanya kazi na kiongozi ambaye ana maono mazuri kwa wananchi,” akasema.

Wakiongea kwenye uzinduzi wa kikundi chao katika Hoteli ya Redbrick iliyo Majengo, wanasiasa hao walisema waliamua kushirikiana ili kuendeleza azma yao.

“Tunataka kuleta mabadiliko ya uongozi hapa Mombasa, hatutakubali kutawaliwa na vyama tena,” alisema mwaniaji wa kiti cha udiwani katika Wadi ya Tononoka, Bw Ibrahim Dube.

Bw Dube alisema wagombea huru wa Urais wameanza kuwafuata ili waweke mkataba wa mawaelewano.

“Lakini hatujaweka mkataba bado. Mgombea huru huwa hana doa sababu chama hakiwezi kumshawishi kufanya maovu,” alisema Bw Dube.

Kikundi hicho kina wanachama 35 ambao walihama UDA baada ya kukosa kupewa tikiti za uwaniaji viti.

Kulingana nao, hatua ya UDA kukabidhi tikiti za moja kwa moja huenda ikafanya Dkt Ruto kushindwa kupata kiti chochote cha siasa Mombasa kwa sababu wale waliobaki upande wake hawafanyi kampeni.

“Wanamgojea aje Mombasa ndio wafanye kampeni. Walitubandua kwa sababu walijua tuna nguvu mashinani. Shida ni uongozi wa UDA eneo la Pwani,” aliongeza Bw Dube.

Bi Joyce Obengele, mwaniaji wa kiti cha Shanzu alisema wanawake hawakupewa nafasi za uongozi na vyama vyote vya kisiasa.

“Ndio maana wanawake wegi tunagombea viti vya kisiasa kama wagombea huru,” aliongeza.

  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Usiwe tofauti pekee wakati wa saumu,...

Siku 96 Uhuru kujikuna kichwa kabla kustaafu

T L