• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Siku 96 Uhuru kujikuna kichwa kabla kustaafu

Siku 96 Uhuru kujikuna kichwa kabla kustaafu

NA LEONARD ONYANGO

HUKU muda wa Rais Uhuru Kenyatta madarakani ukielekea kutamatika, kiongozi wa taifa ana siku 96 zinazotajwa na wachanganuzi wa siasa kama za kukabiliana na mawimbi ya bahari kuu.

Wadadisi hao wanasema kati ya masuala makuu ambayo yanamzonga Rais Kenyatta mawazo akijiandaa kufunganya virago kwenda nyumbani Gatundu ni kuhusu itakuwaje iwapo Naibu Rais William Ruto atashinda urais na atakavyoacha taifa kiuchumi.

Wadadisi wanasema suala la kumpenyeza mwaniaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya pamoja na kutorokwa na wandani wake ni masuala mengine yanayomkosesha usingizi.

“Tofauti na Rais Daniel Moi ambaye chaguo lake la mrithi, ambaye alikuwa Uhuru lilikumbatiwa na watu wa Rift Valley mnamo 2002, chaguo la Rais Kenyatta ambaye ni Bw Odinga, linaonekana kukataliwa na wengi katika ngome yake ya Mlima Kenya. Hali hiyo inampa rais wasiwasi mkubwa kwani alidhani kuwa watu wa Mlima Kenya wangekumbatia Bw Odinga bila pingamizi,” anasema Bw Javan Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Mkurugenzi wa Masuala ya Uchaguzi wa Jubilee na Mbunge wa Kieni, Kanini Kega anakiri kwamba washirika wa Rais Kenyatta wamekuwa na kibarua kigumu kuuza Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Odinga amekuwa akifanya mikutano na wawaniaji wa viti mbalimbali wa Azimio katika kaunti za Mlima Kenya katika juhudi za kuimarisha ushawishi wake eneo hilo.

Bw Bigambo anasema kuwa Rais Kenyatta anafaa kuweka bidii kumtafutia kura Bw Odinga ili kuepuka aibu ya kukabidhi mamlaka kwa hasimu wake wa kisiasa, ambaye ni Dkt Ruto, sawa na alivyofanya marehemu Moi mnamo 2002 alipoachia usukani Mwai Kibaki.

Wadadisi pia wanaonya kuwa hali ngumu ya kiuchumi inayoendelea nchini, ambapo Wakenya wanahangaika kupata chakula na mahitaji mengineyo ya kimsingi, itafanya Rais Kenyatta kustaafu umaarufu wake ukiwa chini zaidi kuliko rais mwingine yeyote aliyemtangulia akiwemo marehemu Moi.

“Kuna mambo mengi ambayo yamesababisha uchumi kudorora kama vile janga la virusi vya corona na mapigano yanayoendelea nchini Ukraine. Lakini wengi wa Wakenya wanaamini kuwa hali ngumu ya maisha imesababishwa na sera za uchumi za serikali ya Jubilee pamoja na ufisadi. Hivyo, Rais Kenyatta itabidi aweke mikakati ya kuinua uchumi ndani ya miezi mitatu iliyosalia, la sivyo atastaafu akiwa na maadui wengi kuliko marafiki,” anasema Bw Bigambo.

UPWEKE

Mwanasiasa na mdadisi wa masuala ya kisiasa George Mboya anaeleza kuwa Rais Kenyatta pia ana wasiwasi kuhusu hatari ya kujikuta mpweke baada ya kustaafu.

“Wandani wake wa muda mrefu wamemkimbia katika siku za mwisho za urais wake. Je, akistaafu na kuishiwa ushawishi wa kisiasa atabaki na nani?” anasema Bw Mboya akishikilia kuna hatari ya kiongozi wa nchi kupoteza udhibiti wa muungano wa Azimio katika muda wa mwaka mmoja pekee iwapo Bw Odinga ataibuka mshindi wa urais.

Kwa sasa Rais Kenyatta, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa viongozi wa muungano huo unaojumuisha vyama 26 watasalia pamoja hadi Agosti 9.

Tayari chama cha Pamoja African Alliance (PAA) chake gavana wa Kilifi Amason Kingi na Maendeleo Chap Chap cha Gavana wa Machakos Alfred Mutua vimetishia kujiondoa ndani ya Azimio vikidai kutengwa.

Chama cha Wiper pia kimetishia kujiondoa iwapo kinara wake Bw Kalonzo Musyoka hatateuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Wagombeaji huru waungana

TAHARIRI: Atakayeshinda urais asuluhishe tatizo la ardhi

T L