• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 1:33 PM
Wajackoyah aahidi kuimarisha ufugaji wa nyoka akichaguliwa rais

Wajackoyah aahidi kuimarisha ufugaji wa nyoka akichaguliwa rais

NA SAMMY WAWERU

NITAZINDUA ufugaji wa nyoka nchini endapo nitaibuka mshindi kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao Agosti 9, ameahidi Prof George Wajackoyah.

Prof Wajackoyah anawania urais kwa tikiti ya Roots Party of Kenya, na amesema ufugaji wa nyoka utalenga kutibu majeraha ya walioumwa na wanayama hao hatari.

Akielezea kusikitishwa kwake na visa vya watu wanaoumwa na nyoka na hata baadhi kufariki, alisema Kenya hutegemea dawa kutoka nje ya nchi ilhali tiba.

“Kenya ina nyoka wengi, tutawakamata na kufuga. Tuvune sumu yake na kuitumia kutibu walioumwa,” Prof Wajackoyah akaelezea.

Alisema hayo Jumatano jioni, katika mahojiano na runinga ya Citizen.

Alitaja eneo la Ukambani na Baringo, kama yanayoshuhudia visa vya watu kuumwa na nyoka akisisitiza wanyama haohao wanapaswa kutumika kama matibabu.

Kauli ya mgombea huyo wa urais imezua mjadala mitandaoni, baadhi wakimtaja kama mwanasiasa mkwasi wa utani.

“Na bado hajagusa chura, ninampenda bure tu,” Faith Masinde akaandika katika Facebook.

“Huyu ana ajenda moto moto,” Patrick Kibor akachangia.

“Inawezekana, anaonekana kuwa na hekima,” @Gabriel Bwire akaandika katika Twitter.

Wengine nao hawakuchelea kumcheka, wakidai Prof Wajackoyah ni kiongozi mcheshi.

“Ati ufugaji wa nyoka? Hahaha…” @Churchill Mugosero akaandika.

Si kisa cha kwanza mwaniaji huyo wa urais kuchochea mdahalo kugaragazwa mitandaoni, akirejelea pendekezo lake la awali kukuza marijuana maarufu kama bangi endapo ataibuka kidedea.

  • Tags

You can share this post!

Afrika Kusini yaanza mikakati ya kurasimisha Kiswahili

Jinsi Kwaya ya Makuburi ilivyoburudisha maelfu ya watu...

T L