• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Wajackoyah kutumia bangi, nyoka na mbwa kukwamua Kenya kutokana na umaskini

Wajackoyah kutumia bangi, nyoka na mbwa kukwamua Kenya kutokana na umaskini

NA LEONARD ONYANGO

MWANIAJI urais wa chama cha Roots, George Wajackoya atapatia kipaumbele kilimo cha bangi, ufugaji wa nyoka na mbwa katika juhudi za kuinua uchumi wa nchi iwapo atachaguliwa Agosti 9.

Prof Wajackoya katika manifesto yake iliyozinduliwa Alhamisi katika jumba la KICC, Nairobi, alisema shamba la ekari 583,000, ambalo ni sawa na Kaunti ya Nyeri, linaweza kuletea Kenya Sh 9.2 trilioni kwa mwaka.

“Bangi inavunwa mara mbili kwa mwaka, hivyo nchi itakuwa na pato kubwa. Tunaweza kujenga barabara mbili za ghorofa kama ile ya Nairobi katika kila kaunti kutokana na kilimo cha bangi,” akasema Prof Wajackoya.

MLIMA KENYA

Kulingana na kiongozi huyo wa Roots, bangi inaweza kufanya vyema katika eneo la Mlima Kenya.

Kwa sasa ni marufuku kukuza na kuuza bangi humu nchini. Watu wanaopatikana na bangi wanaweza kuhukumiwa hadi kifungo cha maisha gerezani.

Lakini Prof Wajackoya ameahidi kufutilia mbali sheria hiyo ili kuhalalisha kilimo cha bangi na kuuza ng’ambo.

Msomi huyo wa sheria pia anaamini kuwa sumu ya nyoka itasaidia kuinua mapato ya Kenya: “Serikali yangu itapatia kipaumbele ufugaji wa nyoka. Chupa ndogo ya sumu ya nyoka aina ya swila, kwa mfano, inauzwa kwa Sh600,000,” akasema Bw Wajackoya.

Serikali ya Roots pia itapatia kipaumbele ufugaji na usafirishaji wa nyama ya mbwa ng’ambo.

Kulingana na Prof Wajackoya, nyama ya mbwa ni ghali zaidi ikilinganishwa na nyama ya mbuzi au ng’ombe: “Kilo moja ya nyama ya ng’ombe au mbuzi inagharimu Sh400, lakini nyama ya mbwa inauzwa kwa Sh2,400 kwa kilo katika nchi za Mashariki ya Kati.”

WAFISADI KUNYONGWA

Manifesto hiyo pia inaahidi kubadilisha sheria ili kuruhusu kunyongwa kwa maafisa wa umma wanaoiba fedha za umma.

Pia Prameahidi kufuta maandishi au michoro ya Wachina iliyo katika Reli ya Kisasa (SGR).

“Wakenya watafanya kazi kwa siku nne pekee kwa wiki na wikendi itakuwa siku tatu Ijumaa, Jumamosi na Jumapili. Wakenya watakuwa wanalipwa mishahara yao kila baada ya wiki mbili,” akasema Bw Wajackoya.

ISIOLO KUWA JIJI KUU

Serikali ya Wajackoya pia imeahidi kuwa itahamisha mji mkuu wa Kenya kutoka Nairobi hadi Isiolo ambapo anasema ni katikati mwa nchi.

“Tutarejesha makwao raia wa kigeni wasio na kazi humu nchini,” inasema manifesto hiyo.

Chama cha Roots pia kimeahidi kuanzisha majimbo manane humu nchini ambayo yatajifanyia maamuzi.

Uzinduzi wa manifesto ya Prof Wajackoya ulikuwa na mbwembwe za kila aina ikiwemo muziki wa Reggae ulioporomoshwa katika ukumbi.

  • Tags

You can share this post!

Arama asukumwa jela miezi sita

KASHESHE: ‘Nimekoma’

T L