• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Wakenya wabebe mzigo wa mafuta ghali bila kulalamika – Moses Kuria

Wakenya wabebe mzigo wa mafuta ghali bila kulalamika – Moses Kuria

Na PETER MBURU

Mbunge mbishi wa Gatundu Kusini amewaghadhabisha Wakenya, baada ya kusema kuwa hawezi kuwatetea kutokana na kupandishwa kwa bei ya mafuta, kwani alipitisha bajeti ya kuyapandisha.

Bw Kuria, kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema hawezi kulia na Wananchi, akiwataka kubeba mzigo wa ushuru bila kulalamika, jambo lililoibua hasira tele na kuwafanya Wakenya kumlaani.

“Mimi ni mwanachama wa kamati ya kukadiria na kutunga bajeti bungeni, nilipiga kura kupitisha bajeti ya zaidi ya Sh3trilioni na kama naibu mwenyekiti wa kamati ya usafiri, ujenzi na kazi za umma niliunga mkono kikamilifu Sh179bilioni kujenga barabara bora, Sh58bilioni kugharamia reli ya SGR kutoka Nairobi hadi Naivasha na mabilioni ya pesa zingine kwa ujenzi wa nyumba,” akasema Bw Kuria.

“Niliwapa pesa kukamilisha ujenzi wa soko zenu zilizokwama, kuendesha shughuli za afya, kukamilisha miradi 58 mabwawa ya unyunyiziaji maji, hamkunikosoa. Hamkujali nilipotoa pesa, kwa hivyo siwezi kuja kulia nanyi kuhusu kupandishwa kwa ushuru wa asilimia 16 kwa mafuta. Nitakuwa najifanya,” mbunge huyo akasema.

Aliendelea kuwalaumu wabunge wanaoteta kuhusu kupandishwa kwa ushuru huo kuwa wanajifanya, akiwataka kusita kuwapumbaza Wakenya.

Lakini semi za Bw Kuria zilikumbana na hasira kutoka kwa Wakenya, wakidai kuwa kupandishwa ushuru ni kuongeza nafasi za pesa za umma kuzidi kuibiwa.

“Kuna baadhi ya miradi ambayo hatuihitaji, kama mradi wa barabara kuu ya kutoka Nairobi kwenda Mombasa ilhali reli ya SGR imekamilika juzi tu,” akasema Jeffrey Koech.

“Kwa hivyo hata wewe hukujua pale pesa za kugharamia miradi unayotaja zingetoka?” akataka kujua CK Yuri.

“Hamuwezi kufadhili miradi yote hii kutoka mifuko ya masikini, pia nyinyi hamkutuuliza miradi ambayo inafaa kutiliwa maanani kwanza,” akasemaXavier Kiwara.

“igieni bajeti kile tulicho nacho, sio kilicho katika mifuko yaw engine. Ikiwa hatuwezi kugharamia, bado hatuhitaji,” Kipkurui Kemoi akasema.

You can share this post!

KERO LA NAULI: Wakenya waanza kuumia

TSC yaajiri walimu 8,000

adminleo