• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Waliomrarua Raila sasa wamnyenyekea

Waliomrarua Raila sasa wamnyenyekea

Na BENSON MATHEKA

Maisha ya kisiasa ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga yamebadilika pakubwa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao unapokaribia waliokuwa wakimpinga katika chaguzi zilizotangulia wakimsifu na kuunga azma yake ya urais.

Miongoni mwao wametangaza hadharani kuwa ndiye anayefaa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta atakapoondoka mamlakani mwaka ujao.

Mnamo Ijumaa wiki jana, Bw Odinga alitangaza kuwa atagombea urais siku moja baada ya mabwenyenye wa eneo la Mlima Kenya kuidhinisha azma yake wakimtaja kama rais wa tano wa Kenya anayesubiri kuingia mamlakani.

Kwenye chaguzi kuu za 2007, 2013 na 2017, matajiri hao walitumia ushawishi wao kumpinga Bw Odinga wakidai akiingia mamlakani, angeweka sera za kuporomosha biashara zao. Kulingana na mchanganuzi wa siasa Peter Kariuki, handisheki ya Bw Odinga na Rais Kenyatta miaka minne iliyopita imebadilisha msimamo wa wengi kuhusu waziri mkuu huyo wa zamani.

“Ilileta utulivu nchini baada ya ghasia zilizokuwa zimeathiri biashara za matajiri hao. Sasa wanamuona kama anayeweza kulinda maslahi yao,” asema Kariuki.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, wapinzani wa Bw Odinga, akiwemo Bw Rais Kenyatta walikuwa wakimpaka tope lakini wakati huu wanammiminia sifa.

Mnamo Desemba 12, Rais Kenyatta alimsifu Bw Odinga kwa kumpa ushauri kuhusu ujenzi wa bustani ya Uhuru Gardens.

Bw Kariuki anasema wanasiasa wengi wamebadilisha nia na kumuunga Bw Odinga kwa kuwa wanahisi ndiye anayeweza kuunganisha nchi na kulinda maslahi yao.

“ Wanasiasa kama Maina Kamanda ( mbunge wa kuteuliwa,, Jubilee) na Gavana Francis Kimemia wa Nyandarua ambao walikuwa wakimpiga vita Bw Odinga kwa miaka mingi sasa wanamsifu na kuunga azima yake,” asema.

Bw Kimemia alikuwa katibu wa usalama wa ndani kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 ambaye alikuwa msitari wa mbele kutetea serikali dhidi ya malalamishi ya Bw Odinga kuhusu madai ya wizi wa kura.

Mnamo Novemba 29 mwaka huu, Bw Kimemia alitangaza kuwa anaunga azima ya Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya.

“Yale tuliyofanya na kusema kumhusu baba miaka iliyotangulia yalitokana na siasa tu,” alikiri Bw Kimemia ambaye amemwalika kaunti yake mara mbili mwaka huu kumpigia debe.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho ambao kabla ya 2018 walikuwa wakimkosoa vikali Bw Odinga na kutumia polisi kuvunja mikutano na maandamano yake, sasa wanaunga azma yake ya kuwa rais wa tano wa Kenya. Mnamo Oktoba 2022 akiwa Kisii, Bw Matiang’i alisema atapigia debe azma ya urais ya Bw Odinga.

“Hamtarajii niongoze jamii yangu pasipo na matumaini. Mahali baba yupo ndipo niko kwa kuwa ndiko rais yupo,” alisema Bw Matiang’i na kutangaza kuwa aliacha kugombea urais ili kumuunga Bw Odinga.

Alishadidia kauli hiyo Ijumaa akiwa Kisumu kwa kusema hajuti kumuunga Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya.

Bw Kibicho, ambaye 2017 alikabili Bw Odinga akisema polisi walikuwa na vitoa machozi vya kutosha kuvunja maandamano, amekuwa akihakikisha kiongozi huyo wa ODM anapata ulinzi wa hali ya juu kokote anakozuru.

Kabla ya 2018, Bw Odinga alikuwa akilaumu maafisa wa usalama na ujasusi kwa kutumiwa kuvuruga kampeni zake na kuiba kura hali ambayo ni tofauti wakati huu anapogombea urais kwa mara ya tano.

Mnamo Ijumaa, aliandamana na Rais Kenyatta kufungua kampuni ya kutengeneza meli ya Kenya Shipyard Limited, Mombasa ambayo iko chini ya Jeshi la Kenya.

“Idara za usalama zinaonekana kuwa na maagizo ya kuhakikisha mambo ya Bw Odinga yako shwari. Hii ni tofauti na chaguzi za awali ambapo alikuwa akipokonywa walinzi,” asema mdadisi wa siasa Jerome Nyaberi.

Kwa wakati huu, Bw Odinga anafanya kampeni zake maeneo ya Mlima Kenya bila kuvurugwa tofauti na chaguzi za awali alipokuwa akinyimwa kununua chakula katika hoteli eneo hilo.

You can share this post!

Mkenya Shoaib Vayani achaguliwa naibu rais ulengaji shabaha...

Matumaini tele daraja la Ngoliba likikaribia kukamilika

T L