• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 10:50 AM
Matumaini tele daraja la Ngoliba likikaribia kukamilika

Matumaini tele daraja la Ngoliba likikaribia kukamilika

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ngoliba Thika Mashariki, na eneo la Murang’a watapata afueni wakati ujenzi wa daraja la kisasa utakapokamilika.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, daraja hilo limekuwa halifanyi kazi baada ya kubomoka wakazi wakibaki kuhangaika.

Baadhi ya shughuli zilizoathirika ni usafiri wa bodaboda, masomo ambapo wanafunzi walitatizika kutoka upande mmoja hadi mwingine, na ulishaji mifugo ambapo wakazi hao walikosa kupeleka mifugo kwa malisho.

Baada ya kupitia masaibu hayo yote, wakazi wa Ngoliba walilazimika kutumia boti kama njia moja ya usafiri huku wakitozwa nauli ya kuvushwa.

Bw Justus Musila mkazi wa Ngoliba, alieleza kuwa kwa kila mmoja kuvuka upande wa pili ni sharti alipe ada ya Sh20.

Halafu wafanyabiashara kuvukishwa upande wa pili wanalipa Sh50 pamoja na mizigo yao.

” Sisi kama wakazi wa eneo hili tumepitia masaibu mengi kwa sababu mashua zinazovusha watu ni tatu pekee na kwa hivyo zinachukua muda kutosheleza mahitaji ya kila mmoja,” alisema Bw Musila.

Alisema wanafunzi pia huchelewa shuleni kila mara kwa sababu ya kuweka foleni ili kungoja kuvushwa hadi upande wa pili.

Matumizi ya boti kuvuka kutoka ng’ambo moja hadi nyingine. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Naye Bi Annah Syombia alisema wanawake hupitia changa moto tele wanapovuka eneo hilo kwa sababu ya kupoteza muda mwingi wakingoja kuvuka.

“Wakati daraja jipya litakapoanza kutumika rasmi bila shaka biashara nyingi zitanawiri na wakazi wa Ngoliba na maeneo ya Murang’a watanufaika pakubwa,” alifafanua Bi Syombia.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘ Jungle’ Wainaina alisema tayari aliwasiliana na halmashauri ya kuunda barabara (KERA) ambao walikubali kuharakisha ujenzi wa daraja hilo.

Alieleza kuwa halmashauri hiyo imesaidia kiasi fulani kugharimia ujenzi huo kwa kutoa vyuma vya ujenzi.

Hata hivyo, alisema gharama yote ya mradi huo itakuwa takribani Sh5 milioni.

“Wakazi wa Ngoliba na Murang’a wamepata shida kubwa huku biashara nyingi zikikwama,” alifafanua mbunge huyo.

Alieleza kuwa chini ya miezi mitatu ijayo, daraja hilo litakuwa limekamilika na wakazi wataendelea na shughuli zao kama kawaida.

Alisema wanafunzi na wakazi wengine wa eneo hilo wataendesha mambo yao kwa njia inayostahili bila kutozwa chochote wakati wa kupitia kwenye daraja hilo.

Wakazi wengi waliohojiwa waliishukuru serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kwa kuingilia kati na kuona ya kwamba shida za wakazi wa Ngoliba zinatatuliwa mara moja.

Mto wa hapo umekuwa tisho kwa wakazi wa Ngoliba kwa sababu viboko wanaishi humo.

  • Tags

You can share this post!

Waliomrarua Raila sasa wamnyenyekea

Barcelona wapaa hadi nafasi ya saba baada ya kupepeta Elche...

T L