• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Wamatangi avuliwa wadhifa wa seneti kwa kujiunga na Hasla

Wamatangi avuliwa wadhifa wa seneti kwa kujiunga na Hasla

Na CHARLES WASONGA 

CHAMA cha Jubilee kimemvua Seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi wadhifa wake wa Kiranja wa Wengi katika Bunge la Seneti siku chache baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kuwa amejiunga na kambi ya Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Jumamosi Machi 13, 2022, Bw Wamatangi alipokelewa rasmi ndani ya chama cha UDA katika mkutano wa kisiasa ulioongozwa na Dkt Ruto katika uwanja wa michezo mjini Thika.

Katika mkutano huo, seneta huyo alitangaza kuwa atashindania tiketi ya UDA ili kuwania kiti cha ugavana wa Kiambu katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Duru zilisema kuwa hata kabla ya kutangaza kuhamia UDA, Bw Wamatang’i alikuwa amelipa ada ya Sh500,000 ili kushiriki kura ya mchujo kuwania ugavana wa Kiambu.

Kwenye barua iliyoandikiwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni mnamo Machi 16, 2022,  Bw Wamatang’i pia ameondolewa kutoka kwa nyadhifa zozote za uongozi anazoshikilia katika Seneti kwa misingi ya kuwa mwanachama wa Jubilee.

“Hatua hii imechukuliwa dhidi yako ulipotangaza waziwazi katika mkutano wa Kenya Kwanza mjini Thika mnamo Machi 13, 2022 kuwa utawania ugavana wa Kiambu kwa tiketi ya UDA. Kwa hivyo, inafasiriwa kuwa umehama Jubilee kulingana na kipengele cha 5 cha katiba ya chama chetu,” Bw Kioni akasema.

Katibu huyo mkuu alisema ni baada ya Bw Wamatangi kutangaza hadharani kujiunga na UDA ambapo Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ilifanya kikao mnamo Machi 14 kulizungumzia suala hilo.

“Kwa hivyo unaombwa kujibu barua hii kufikia Machi 17, jioni ukisema ikiwa unakubaliana na uamuzi huu. Ikiwa muda huo utakamilika na chama hakitakuwa kimepokea majibu yoyote kutoka kwako kusema kuwa haukubaliani na uamuzi huo, Spika wa Seneti Ken Lusaka anajulishwa rasmi kuhusu mabadiliko hayo,” Bw Kioni akasema.

Nakala za barua hiyo zilitumwa kwa Bw Lusaka na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Nchini Anne Nderitu.

Bw Wamatang’i sasa atang’ang’ania tiketi ya kupeperushwa bendera ya UDA katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kiambu katika kura ya mchujo itakayofanyika kuanzia Aprili 9 hadi Aprili 22.

 Atashindana na Patrick Wainaina (Mbunge wa Thika Mjini), aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu Baba Yao na Spika wa Bunge la Kiambu Stephen Ndichu.

  • Tags

You can share this post!

Vigogo wa kizazi kipya wadhibiti Pwani kisiasa

Kero ya dimbwi la majitaka karibu na majumba ya makazi...

T L