• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Vigogo wa kizazi kipya wadhibiti Pwani kisiasa

Vigogo wa kizazi kipya wadhibiti Pwani kisiasa

NA WAANDISHI WETU

ENEO la Pwani linazidi kuibuka kama ukanda ambapo wanasiasa wa kizazi kipya wanajizatiti kuwa na ushawishi mkubwa.

Ikilinganishwa na sehemu nyingine nyingi za nchi ambapo ushawishi wa kisiasa huwa mikononi mwa viongozi ambao wamekuwa ulingoni kwa miongo mingi, kaunti za Pwani zimeonyesha hali ambapo walio na ushawishi mkubwa ni wale wa kizazi kipya.

Baadhi ya wanasiasa hao ni magavana Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Granton Samboja (Taita Taveta), na Salim Mvurya (Kwale).

Mbali na hawa, kuna wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Mishi Mboko (Likoni), Khatib Mwashetani (Lungalunga), Abdulswamad Nassir (Mvita) miongoni mwa wengine.

Licha ya wanasiasa hao kuonyesha ukakamavu na weledi wa kisiasa, maswali yangali yanaibuka kuhusu uwezo wao wa kufanikisha utatuzi wa changamoto sugu ambazo zimekuwa zikikumba ukanda wa Pwani kwa miaka na mikaka.

Kwa mujibu wa wachanganuzi wa kisiasa, viongozi wa kizazi kipya wangali wana safari ndefu katika juhudi za kukidhi maslahi makuu ya Wapwani.

Hii ni ikizingatiwa jinsi matatizo hayo huibuka kila wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, ukiwemo wa mwaka huu.

Mchanganuzi wa kisiasa, Prof Hassan Mwakimako, anasema kuwa kwa sasa hakuna kiongozi wa kizazi kipya ambaye amedhihirisha uwezo wa kuwafikia wanasiasa wa zamani wa Pwani kama vile Karisa Maitha, Ronald Ngala na Sharif Nassir.

“Hakuna kiongozi mwenye ushupavu wa Ngala au Maitha. Sisi tuliobaki ni watu wenye tamaa ya mamlaka na vyeo na pesa. Lakini uongozi wa utumishi bado haujafikiwa na viongozi waliopo sasa,” akasema.

Wadadisi wamesema kuwa mojawapo ya sababu zinazochangia viongozi wa kizazi kipya kushindwa kufanikisha mahitaji ya wakazi wa Pwani kikamilifu ni jinsi wanavyokosa kuungana.

Juhudi nyingi zimekuwa zikiwekwa na wanasiasa eneo hili kuungana lakini zote zimegonga mwamba.

Miaka michache iliyopita, viongozi kadha wa Pwani walionyesha nia ya kutaka kuungana chini ya chama kimoja ila wakasambaratika.

Juhudi hizo zilikuwa zikiendeshwa na Gavana Kingi, ambaye hatimaye aliamua kuunda chama chake cha Pamoja African Alliance na kujitenga na Chama cha ODM alichokuwa ametumia kushinda ugavana kwa vipindi viwili.

Bw Joho aliamua kusalia ODM ambapo yeye ni naibu kiongozi, huku Bw Mvurya aliyechaguliwa kupitia kwa ODM 2013 na Jubilee 2017 akiamua kuungana na Naibu Rais William Ruto katika Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Kwa upande mwingine, Bw Samboja ambaye alichaguliwa kupitia Chama cha Wiper amekuwa akijumuika na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika kampeni zake za hivi karibuni.

Bw Kingi amekuwa akilazimika kujitetea dhidi ya madai kwamba alitaka kuleta pamoja wanasiasa wa Pwani kwa maslahi yake ya kibinafsi, akisisitiza kuwa mpango wake ulikuwa ni kutafuta njia bora ambayo Wapwani wanaweza kutumia kupigania nafasi yao katika meza ya serikali ya kitaifa.

Akizungumza hivi majuzi katika Kaunti Ndogo ya Rabai, gavana huyo alionya kuwa Pwani itaendelea kutumiwa vibaya na wanasiasa iwapo viongozi hawatazinduka kutoka usingizini.

“Kila eneo limeamka, na watu wanapanga mikakati kuhusu jinsi watakuwa na usemi na kunufaika kutoka kutokana na serikali ya kitaifa. Lazima tujipange ili kuhakikisha ahadi zinazotolewa wakati wa kampeni na viongozi wanaoomba kura zetu zitatekelezwa baada ya uchaguzi. Bila hilo, jamii za Wapwani zitaendelea kukosa sauti,” akasema.

Kulingana na Bw Kingi, vyama vingi vinavyotambuliwa kuwa vya kitaifa vina mizizi yavyo katika jamii mbalimbali na hivyo basi Pwani pia inastahili kufuata mkondo huo.

Ripoti za Kennedy Kimanthi, Farhiya Hussein na Valentine Obara

  • Tags

You can share this post!

Familia kadhaa zakosa miili ya jamaa zao Yala

Wamatangi avuliwa wadhifa wa seneti kwa kujiunga na Hasla

T L