• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Wandani wakuu wa Joho wang’ang’ania useneta

Wandani wakuu wa Joho wang’ang’ania useneta

NA BRIAN OCHARO

WANDANI wakuu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho watapambana katika kinyang’anyiro cha useneta ambacho kimevutia zaidi ya wagombea sita.

Aliyekuwa Katibu wa Kaunti Hamisi Mwaguya na kakake gavana huyo Bw Mohamed Amir wote wanakimezea mate kiti hicho chini ya Muungano wa Kenya Kwanza.

Bw Amir alikuwa akihudumu kama mkuu wa askari wa kaunti.

Bw Mwaguya na Bw Amir walijiunga na chama cha naibu rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).

Wawili hao Alhamisi walikosoa utawala wa gavana Joho kwa kukosa kuanzisha ajenda ya maana ya maendeleo inayoweza kubadilisha mji huo.

Wakizungumza huko Changamwe wakati wa mkutano wa Muungano wa Kenya Kwanza, wanasiasa hao wawili waliwataka wapiga kura wa Mombasa kurekebisha uongozi mzima wa kaunti kwa kuwapeleka nyumbani viongozi ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

“Kenya Kwanza ndiyo suluhu la pekee kwa matatizo ambayo yanaisumbua nchi na mji huu wa Mombasa. Tunawaomba muwe makini katika uchaguzi wa Agosti 8, 2022,” Amir alisema

Viongozi hao pia walisema kuwa wanasiasa wa Pwani wametia saini mkataba na Dkt Ruto na kikosi cha Kenya Kwanza kufufua uchumi wa eneo hilo iwapo naibu wa rais atashinda uchaguzi wa Agosti.

Walisema mkataba huo utahakikisha shughuli muhimu za bandari ya Mombasa ambazo zimeathiriwa na reli ya kisasa (SGR) zimerejeshwa.

Wanasiasa hao walishutumu utawala wa kaunti hiyo kwa kukosa kukomesha, walichotaja kuhamisha huduma za bandari kutoka Pwani hadi Naivasha, jambo ambalo wanadai limeua biashara ya uchukuzi na uchumi wa eneo hilo kwa jumla.

“Haya yote yatarejeshwa chini ya uongozi wa Kenya Kwanza,” alisema Mbunge wa Nyali Mohamed Ali, ambaye pia alihudhuria mkutano huo.

Takriban wagombea sita wametangaza nia yao ya kumvua nyadhifa Mohamed Faki ambaye anashikilia kiti hicho kwa sasa. Seneta Faki ametangaza kuwa atatetea kiti chake kupitia tikiti ya chama cha ODM.

Mfanyabiashara wa Mombasa Hisham Mwidau ni mmjoa wa wanaisasa ambao wanamezea mate kiti hicho cha useneta.

Bw Mwidau ametangaza nia ya kuwania kiti hicho kupitia tikiti ya chama cha ODM.

Mfanyabiashara huyo, hata hivyo, atachuana na Bw Faki kwenye mchujo wa ODM kutafuta tiketi ya chama hicho.

Uongozi wa chama hicho mjini Mombasa umewahakikishia wanaowania tikiti ya chama hicho mchujo huru, wa haki na wa kuaminika.

Viongozi hao wameeleza kuwa hakuna mgombea yeyote aliyeidhinishwa na uongozi wa chama hicho kwa wadhifa wowote wa kuchaguliwa.

Pia, chama hicho kimesisitiza kuwa wanachama mjini Mombasa ndio watakaoamua kupitia uteuzi wawaniaji watakapeperusha bendera yake katika nyadhifa zote za uchaguzi.

Bw Faki na Bw Mwidau watamenyana kwa mara ya pili katika vita vya kuwania kupitia kwa tiketi ya chama hicho.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Bw Mwidau kujaribu bahati yake kutafuta tikiti ya chama hicho. Bw Mwidau alishindwa na Bw Faki kwenye mchujo wa chama hicho mnamo 2017. Lakini anashikilia kuwa sasa amepata tajriba na amejizolea umaarufu miongoni mwa wapiga kura.

Na pia mnamo 2002, mfanyabiashara huyo aliwania kiti cha ubunge cha Likoni bila mafanikio. Aliipoteza baada ya kushindwa na marehemu Masoud Mwahima.

Lakini Bw Mwidau anasema yakati zimebadilika na kueleza matumaini yake kuhusu kujinyakulia tikiti ya ODM

Kiti hicho cha useneta kimevutia takriban wagombea sita wanaotaka kumvua madaraka Bw Faki.

Wengine wanaowania kiti cha useneta ni pamoja na John Mcharo, aliyekuwa naibu gavana wa Mombasa Hazel Katana na Abdulsalam Kassim.

Bw Amir alijiunga na UDA mwaka 2021. Bw Amir na Bw Mwaguya wote wanatafuta tikiti ya chama cha UDA na kwa hivyo watapambana katika uteuzi.

You can share this post!

TAHARIRI: Adhabu kwa Gor Mahia iwe funzo kwa timu zinazozua...

Uhuru akuza wanasiasa kizazi kipya Mlimani

T L