• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
TAHARIRI: Adhabu kwa Gor Mahia iwe funzo kwa timu zinazozua ghasia viwanjani

TAHARIRI: Adhabu kwa Gor Mahia iwe funzo kwa timu zinazozua ghasia viwanjani

NA MHARIRI

BAADA ya ghasia kuzuka katika uwanja wa MISC Kasarani wakati timu ya Gor Mahia ilipokuwa ikicheza na Vihiga Bullets mnamo Februari 13, sasa uamuzi umefikiwa baada ya uchunguzi kufanywa na Kamati Shikilizi ya masuala ya soka nchini.

Klabu ya Gor imepatikana na makosa ya kutohakikisha kulikuwa na usalama wa kutosha kwa klabu ya Bullets kwa kuwa wao ndio walikuwa wenyeji wao. Kufuatia hatia hiyo, klabu hiyo imepokonywa ushindi wa mechi hiyo na wapinzani wao wakakabidhiwa pointi tatu,

Aidha mashabiki wa Gor Mahia wamepigwa marufuku kuhudhuria mechi mbili zijazo za klabu hiyo ambazo zitachezewa nyumbani kwenye uwanja wa Moi, Kisumu. Mechi hizo ni kati ya Gor na Kenya Police na pia Wazito.

Ikumbukwe kwamba kamati inayosimamia viwanja humu nchini ilikuwa imewafungia nje mashabiki na klabu ya Gor Mahia kuhudhuria na kuchezea katika baadhi ya viwanja vya hadhi mijini kufuatia fujo za mwezi uliopita ambazo ziliandamana na uharibifu wa vifaa kama uvunjaji wa lango kuu kama ilivyoshuhudiwa viwanjani Kasarani na Thika Municipal Stadium.

Baada ya kuzuiwa kuchezea katika viwanja vya Nyayo, Moi Kasarani na Thika, Gor ilikuwa imeanza kuandaa mechi zake katika viwanja vya nyumbani Moi, Kisumu na Bukhungu, Kakamega.

Kamati Shikilizi ya Soka nchini kupitia sekritariati yake inafaa kupongezwa kwa kutoa adhabu kali kama hii hata katika uwanja wa nyumbani wa klabu hii kama njia ya kuelezea mashabiki wake kwamba uzuaji fujo ni hati na uhalifu ambao hauruhusiwi popote hata ikiwa ni maeneoni yao.

Vivyo hivyo, klabu ya Vihiga Bullets ni ya kuvuliwa kofia kwa hatua yao ya kuonyesha juhudi zao za kuzuia vita pale ilipokataa kurejea uwanjani kuendelea na awamu ya pili ya mechi hiyo ambapo Gor Mahia ilikuwa ikiongoza kwa bao moja kwa bila.

Ingawa wengi wangekielewa kitendo hicho kama cha uoga wa kuvamiwa na pia kushindwa kwa upande wa Vihiga Bullets, ni busara kuzingatia maantiki ya Waswahili kwamba, ‘Kwa mwoga huenda kicheko, kwa shujaa huenda kilio.’ Timu hizi mbili zingerejea ugani katika mazingira yaliyokuwepo, bila shaka watu zaidi ya watatu waliojeruhiwa siku hiyo, wangeripotiwa.

Hata hivyo, ni jambo la kuhuzunisha kutambua kwamba hakukuwa na usalama wa kutosha wakati ghasia hizi zilizuka katika uwanja huo wa Kasarani, Nairobi.

Wasimamizi wa soka na viwanja nchini wanafaa kushirikiana na wizara ya Usalama wa Ndani kuhakikisha maafisa wa polisi wa kutosha wanatumwa viwanjani wakati timu kubwa zinapochezwa na hasa klabu ambazo zina historia ya kusababisha fujo. Ni vyema kuzuia kuliko kutibu

You can share this post!

VITUKO: Kidosho adai Sanchez ana wivu na Fabinho

Wandani wakuu wa Joho wang’ang’ania useneta

T L