• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wafuasi watishia kuhama UDA baada ya uteuzi wa ukora

Wafuasi watishia kuhama UDA baada ya uteuzi wa ukora

NA WAANDISHI WETU

CHAMA CHA UNITED Democratic Alliance (UDA) kitarudia uteuzi katika eneobunge la Moiben huku malalamishi yakiendelea kote nchini kuhusu mchujo huo ulivyoandaliwa.

Baadhi ya walioshindwa wametishia kuhama chama hicho wakidai walinyimwa haki.

Jana, wawaniaji kadhaa walipiga kambi katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi kulalamika.

Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya chama hicho ilifuta matokeo ya uteuzi wa eneobunge la Moiben uliofanyika mnamo Alhamisi.

Chama hicho kilisema kuwa uamuzi huo uliafikiwa baada ya mala – lamishi kutoka wa wagombeaji wa nyadhifa zote sita.

“Sasa tunawaomba wawaniaji wajiandae kwa marudio. Bodi inawahakikishia wapigakura wa Moiben kuwa bado wana nafasi ya kumteua mgombeaji wanayemtaka kupeperusha bendera ya UDA, katika uchaguzi mkuu ujao,” ikasema taarifa ya bodi iliyosomwa na Afisa Msimamizi wa Uchaguzi katika Kaunti ya Uasin Gishu, Benjamin Kibet.

Baadhi ya wawaniaji ambao wanasaka tiketi ya UDA kwa ajili ya uchaguzi wa Agosti 9 ni Prof Phyliss Bartoo, James Kibor, aliyekuwa Mbunge wa Eldoret Mashariki, Joseph Lagat na Diana Chebet.

Mshindi wa uteuzi huo atapambana na mbunge wa sasa Sila Tiren ambaye atakuwa akitetea wadhifa wake kama mwaniaji huru baada ya kukosa kushiriki uteuzi huo.

Ghasia zilizuka katika kituo kikuu cha kuhesabu kura cha Tac baada ya wafuasi wa wawaniaji kukabaliana na kuwalazimu maafisa wa polisi ku – ingilia kati na kurejesha utulivu.

Seneta Mteule, Bi Millicent Omanga ambaye alikuwa mwakilishi wa afisi kuu katika uteuzi huo, mnamo Ijumaa jioni alisema kuwa chama hicho kingetoa mwelekeo na kuanda mchujo huo upya katika nafasi zote sita za uongozi.

Naye Mwakilishi wa Kike wa Tharaka-Nithi, Beatrice Nkatha na aliyekuwa Gavana Samuel Ragwa wametishia kuhama UDA wakidai uteuzi wa chama hicho ulikumbwa na wizi wa kura.

Bi Nkatha, mwandani wa Naibu Rais William Ruto, alitoa makataa kwa UDA kuyashughulikia malalamishi yao kufikia Jumatatu la sivyo, wahame chama. Mbunge huyo alimwelekezea lawama Gavana Muthomi Njuki akisema alivuruga uteuzi huo ili kuwapendelea wawaniaji anaotaka.

Bi Nkatha alishindwa katika mchujo na Mhadhiri Dkt Beatricke Kathomi ambaye alizoa kura 49,327 dhidi ya 23,860 za mbunge huyo. Naye Diwani wa wadi ya Mukothima, Julius Mwenda Gataya, alimshinda Bw Ragwa kwenye uteuzi wa kiti cha useneta kwa kupata kura 40,746 dhidi ya 33, 742 za gavana huyo wa zamani.

“Inashangaza kuwa hata kura za vituo ambavyo uteuzi haukufanyika, zilijumuishwa kwenye matokeo ya mwisho. Chama hiki kilikuwa imara

hapa lakini tangu ujio wa Njuki, ametwaa usimamizi na kukivuruga, na sasa umaarufu wa Naibu Rais katika kaunti hii unalemazwa,” akasema Bi Nkatha mjini Kathwana.

Katika Kaunti ya Mombasa, kaka wa Gavana Hassan Joho, ambaye alikuwa akiwania kiti cha useneta wa Kaunti ya Mombasa, aliongoza wawaniaji waliokosa tikiti kuhama chama hicho.

Bw Mohammed Amir ambaye alihamia ODM na kujiunga na UDA kwa dhamira ya kuwania useneta kwa chama hicho alifichua masaibu wal – iyokumbana nayo kabla ya mchujo wa chama hicho.

Wawaniaji hao wamedai kwamba walibanduliwa kwenye mchujo na wakuu wa chama hicho.

Ripoti ya Stanley Kimuge, Alex Njeru na Winnie Atieno

  • Tags

You can share this post!

Keter akubali kushindwa na limbukeni wa siasa

Washirika wa Ruto wadai Uhuru na Raila wamemsaliti Kalonzo

T L