• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Watu 8 waorodheshwa kupigwa msasa kubaini anayefaa kuwa mgombea mwenza wa Raila

Watu 8 waorodheshwa kupigwa msasa kubaini anayefaa kuwa mgombea mwenza wa Raila

NA CHARLES WASONGA

KAMATI maalum iliyotwikwa jukumu la kupendekeza mtu anayefaa kuwa mgombea mwenza wa mgombea wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya imeorodhesha majina ya watu waliofaulu katika mchujo wa kwanza.

Miongoni mwao ni kingozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi.

Wengine walioorodheshwa baada ya mchujo huo wa kwanza ni aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Muranga Sabina Chege waliopendekezwa na chama tawala cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Aidha, kamati hiyo, inayoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mifugo Noah Wekesa, imeorodhesha Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho,  aliyekuwa balozi Stephen Tarus aliyependekezwa na chama cha National Liberal Party (NLP) na Charity Ngilu (Narc).

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Sekretariati ya kushirikisha kampeni za Bw Odinga, Dennis Onsarigo, majina ya watu wengine 12 yalikataliwa “kwa sababu yaliwasilishwa na vyama ambavyo haviko ndani ya muungano wa Azimio.”

“Kamati hiyo ilipokea majina ya watu 20 kufikia saa sita za usiku mnamo Alhamisi Mei 5, 2022, muda ambao uliwekwa. Watu waliofuzu watafanyiwa ukaguzi zaidi ilhali waliokataliwa ni kwa sababu walipendekezwa na vyama ambavyo sio tanzu katika Azimio,” akasema Bw Onsarigo katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari aliyoitoa Ijumaa, Mei 6, 2022.

Kutolewa kwa majina hayo manane kunajiri wakati ambapo Bw Musyoka anaendelea kushikilia kuwa hafai kupigwa msasa na kamati hiyo.

Akiongea wakati wa msururu wa kampeni za kupigia debe muungano wa Azimio na mgombeaji wa ugavana wa Mombasa kwa tiketi ya Wiper Mike Sonko, Bw Musyoka alisema kuwa suala la ni nani anafaa kuwa mgombeaji mwenza wa Bw Odinga lafaa kuamuliwa na yeye, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Wakufunzi Mikel Arteta na Jonas Eidevall watia saini...

Seneta aomba msamaha korti kuhusu chuki

T L