• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Wawaniaji wa ugavana Bungoma njia panda kuhusu chama cha kutumia 2022

Wawaniaji wa ugavana Bungoma njia panda kuhusu chama cha kutumia 2022

Na BRIAN OJAMAA

WAWANIAJI mbalimbali wa kiti cha Ugavana katika Kaunti ya Bungoma wamejipata katika njia panda huku wakikosa kuweka hadharani mrengo wanaougemea kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wagombeaji hao akiwemo Gavana wa sasa Wycliffe Wangamati na Spika wa Bunge la Seneti Ken Lusaka, bado hawajaweka bayana iwapo wanaegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga au chama kilichozinduliwa hivi majuzi cha DAP-K ambacho kinahusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa ushindani mkali upo kati ya Bw Wangamati na Lusaka ingawa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kibabii Sophy Waliaula na Peter Khakina pamoja na mfanyabiashara Zacharia Barasa pia wamejitosa ulingoni.

Inadaiwa Bw Wamangati hajui ajiunge na mrengo wa Dkt Ruto ambao utamvunia uungwaji mkono wa wabunge watano wa kaunti hiyo. Wabunge hao ni Didmus Barasa (Kimilili), Mwambu Mabonga (Bumula), John Waluke (Sirisia), Fred Kapondi (Mlima Elgon) na Dan Wanyama (Webuye Magharibi), wote wakiwa katika kambi ya ‘hasla’.

Licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya Ford Kenya, gavana huyo anatafuta chama kingine baada ya kukosana na kiongozi wa chama hicho Moses Wetang’ula ambaye ashatangaza hadharani kuwa atamuunga mkono Bw Lusaka 2022.

“Tusiwadanganye watu wetu. Rais wa Kenya atakuwa Ruto au Raila. Lazima tujihusishe na mrengo ambao utapata ushindi na kuunda serikali,” akasema Bw Wangamati.

Ingawa anaungwa mkono na Bw Wetang’ula, Bw Lusaka amekuwa akisitasita kujiunga na Ford Kenya akihofia kukosa uungwaji mkono wa mrengo unaoegemea DAP-K.

“Tumefikiwa na vyama mbalimbali na bado tunaendelea na mazungumzo. Jambo la muhimu katika kushinda kura ni kusikiliza sauti ya raia,” akasema Bw Lusaka.

You can share this post!

Arsenal washauriwa kumuuza Aubameyang, kutafuta mvamizi...

KIKOLEZO: Wenzetu waliamua kwa dhiki au faraja

T L