• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Maeneobunge 5 yaliyo na kura nyingi sasa kivutio kwa wawaniaji

Maeneobunge 5 yaliyo na kura nyingi sasa kivutio kwa wawaniaji

NA ERIC MATARA

WANASIASA wanaomezea nyadhifa mbalimbali katika Kaunti ya Nakuru wamekita kambi katika maeneobunge matano yaliyo na idadi kubwa ya kura.

Wanasiasa hao wamekuwa wakizunguka katika maeneobunge ya Naivasha, Kuresoi Kusini, Kuresoi Kaskazini, Njoro na Molo kushawishi wakazi huku zikiwa zimesalia siku 48 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Eneobunge la Naivasha lina wapigakura 200,000, kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wawaniaji wa ugavana, useneta na uwakilishi wa wanawake watakaozoa idadi kubwa ya kura katika eneobunge la Naivasha watakuwa na nafasi nzuri ya kuibuka washindi.

Kaunti ya Nakuru ina jumla ya wapigakura milioni 1.1 na maeneo ya Naivasha, Kuresoi, Njoro na Molo ndiyo yataamua washindi.Kwa mujibu wa sajili ya 2022 ya IEBC, maeneobunge hayo kwa pamoja yana wapigakura 500,000.

Wawaniaji wa ugavana wa Nakuru Seneta Susan Kihika (United Democratic Alliance) na Gavana Lee Kinyanjui (Jubilee) wamekita kambi katika maeneo hayo kwa muda wa wiki mbili sasa katika juhudi za kusaka uungwaji mkono.

Bi Kihika amekuwa akizunguka katika maeneobunge ya Naivasha, Kuresoi Kusini, Kuresoi Kaskazini, Njoro na Molo huku akiahidi wakazi vinono kama vile kuwapa fursa za ajira, ujenzi wa miundomsingi, kuwaletea maji safi, ujenzi wa masoko, kuboresha huduma za matibabu, kilimo na utalii.

“Nitahakikisha kuwa Kaunti ya Nakuru inakuwa na maji safi, masoko ya kisasa, huduma bora za matibabu, barabara nzuri,” akasema Bi Kihika alipokuwa akijipigia debe katika Wadi ya Lake View.

Bi Kihika amekuwa akizunguka katika maeneo ya Maella, Olkaria, Lake View, Viwandani na Naivasha Mashariki eneobunge la Naivasha), Lare, Mauche, Mau Narok (Njoro), Kiptagich na Molo kati ya mengineyo.

Naye, Gavana Kinyanjui amekuwa akizindua miradi katika maeneo hayo kuvutia wapigakura.

“Ninaamini kwamba nitachaguliwa tena kwa muhula wa pili ili kukamilisha miradi yangu niliyoanza. Miongoni mwa miradi hiyo ni upanuzi wa miundomsingi na kuunganisha idadi kubwa ya wakazi na huduma za maji,” akasema Bw Kinyanjui alipokuwa akijipigia debe katika eneo la Naivasha.

Kinyang’anyiro cha ugavana katika Kaunti ya Nakuru kwa sasa kinachukuliwa kuwa ubabe wa kisiasa baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Bi Kihika anaungwa mkono na Dkt Ruto huku Gavana Kinyanjui akiegemea upande wa Rais Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Wazee kuamua rais wa tano wa Kenya

TAHARIRI: Maelezo kuhusu wawaniaji wote yaanikwe wazi

T L