• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ana asili ya Kenya

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ana asili ya Kenya

MASHIRIKA na MARY WANGARI

RISHI Sunak aliye na usuli na asili nchini Kenya ndiye Waziri Mkuu mpya wa Uingereza baada ya kuchaguliwa Jumatatu kuwa kiongozi wa chama cha Conservative siku chache baada ya kujiuzulu kwa mtangulizi wake Liz Truss.

Sunak (pichani) mwenye umri wa miaka 42 amekuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Uingereza ndani ya kipindi cha miezi saba.

Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuhudumu vilevile kama waziri kwa zaidi ya miaka miwili, alitangazwa mshindi Jumatatu baada ya mgombeaji wa pekee aliyekuwa amesalia, Penny Mordaunt, kukosa kufikisha kura 100 kutoka kwa wabunge wenzake.

Mordaunt aliripotiwa kuungwa mkono na wabunge 30 huku wabunge wapatao 150 wakimpigia debe Sunak.

“Hizi ni nyakati za mambo tusiyoyatarajia. Licha ya ratiba fupi ya kinyang’anyiro cha uongozi, ni wazi kuwa wenzetu wanahisi tunahitaji jibu leo,” alisema Mordaunt kupitia taarifa.

“Wamechukua uamuzi huu kwa nia nzuri kwa manufaa ya taifa zima.”

Waziri Mkuu wa zamani Boris Johnson alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho Jumapili usiku. Sunak alizaliwa mnamo 1980 katika eneo la Southampton, Uingereza akiwa mwana wa baba Mkenya, Yashvir Sunak na mama yake mwenye asili ya Tanzania, Usa Sunak.

Sunak ambaye asili ya familia yake inatokana na Wapunjabi kutoka India, atakuwa mtu wa kwanza ‘mweusi’ kuwa waziri mkuu wa Uingereza.

Hata hivyo, si Waziri Mkuu wa kwanza kutoka makabila ya walio wachache ikizingatiwa Benjamin Disraeli, mwenye asili ya Kiyahudi aliongoza afisi hiyo mara mbili kati ya 1868 na 1880.

Sunak alizaliwa mjini Southampton, Uingereza mnamo 1980, kama kifungua mimba miongoni mwa watoto watatu.

Baba yake Yashvir Sunak alizaliwa nchini Kenya katika enzi za ukoloni huku mama yake, Usha Sunak akizaliwa Tanganyika. Babu yake Ramdas Sunak, alizaliwa nchini Pakistan kabla ya kuhamia Nairobi mnamo 1935 alipokuwa akifanya kazi kama karani kabla ya kukutana na mke wake Suhag Rani Sunak kutoka Delhi , India mnamo 1937.

Sunak anakuwa kiongozi wa pili mwenye asili ya Kenya, baada ya rais wa zamani wa Amerika Barack Obama, kuongoza taifa lenye ushawishi duniani.

  • Tags

You can share this post!

Mauaji ya kifamilia yatisha

Didmus Barasa yuko huru kuzuru Bungoma

T L