• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wito Karua aongezewe walinzi katika mikutano yake ya kisiasa

Wito Karua aongezewe walinzi katika mikutano yake ya kisiasa

NA GEORGE MUNENE

VIONGOZI wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kutoka Kaunti ya Kirinyaga sasa wanataka mgombeaji mwenza wa muungano huo, Martha Karua, aongezewe walinzi na serikali.

Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Kirinyaga, Bw Mureithi Kang’ara, Jumapili alisema kuna baadhi ya wanasiasa ambao hawafurahishwi na ukakamavu wa Bi Karua anayempigia debe mwaniaji wa Urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga

“Wale ambao wanafanya kampeni dhidi ya Azimio hawafurahishwi na ukakamavu na kujituma kwa Bi Karua katika kumvumisha Bw Odinga eneo la Mlima Kenya na maeneo mengine nchini. Kwa hivyo, anafaa kuhakikishiwa usalama wake kwa kuongezewa maafisa wa polisi ili kumpa ulinzi kwenye mikutano yake ya kisiasa,” akasema Bw King’ara.

Wiki jana, Bi Karua aliondolewa kwa haraka kabla ya kuhutubia umati katika uga wa Gusii, baada ya gesi ya kutoa machozi kurushwa karibu na jukwaa la wageni. Afisa mmoja wa polisi anachunguzwa kutokana na kisa hicho.

Bi Karua awali alikuwa amehutubia mikutano maeneo mbalimbali katika kaunti hiyo akisaka uungwaji mkono kwa Bw Odinga.

Naye Seneta wa Kirinyaga, Bw Charles Kibiru, anayelenga ugavana kama mwaniaji huru, aliahidi kuwa watashirikiana na wanasiasa wengine kuhakikisha kuwa Bw Odinga anazoa kura nyingi eneo la Mlima Kenya.

“Bw Odinga amemtunuku msichana wetu wadhifa wa mgombeaji mwenza na tunafaa kumshukuru kwa kumpa kura nyingi,” akasema Bw Kibiru kwenye mikutano katika miji ya Kutus, Kagio na Kianyaga.

Alimrejelea Bw Odinga kama mwanasiasa mzalendo ambaye atapambana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa nchi.

Naye mwaniaji wa Ugavana Kirinyaga kwa tikiti ya Narc Kenya, Bw Muriithi Kagai, alimpigia Bw Odinga debe na kuwataka wakazi wa Kirinyaga wasiwachague tena wanasiasa waliohudumu kati ya 2017-2022.

“Hatuna dawa katika hospitali zetu na sekta ya kilimo inasimamiwa vibaya. Raia wamekuwa wakiteseka kutokana na uongozi mbaya na tunahitaji viongozi wengine ambao wanazingatia maslahi ya wananchi,” akasema Bw Kagai katika kijiji cha Mukinduri.

  • Tags

You can share this post!

Ajali yaangamiza 3 akiwemo mke wa aliyekuwa mbunge

Ombi la Nyong’o kuendelea kuishi kwa nyumba ghali lazua...

T L