• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Wito makundi ya CSOs yaungane na Azimio kwa mkutano wa Saba Saba

Wito makundi ya CSOs yaungane na Azimio kwa mkutano wa Saba Saba

NA CHARLES WASONGA

WITO umetolewa kwa makundi yote ya mashirika ya kijamii (CSOs) kujitokeza na kuunga mkono mkutano wa Saba Saba ulioitishwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne jioni, mwenyekiti wa vuguvugu la kutetea haki na utawala bora, Yay Network Lobby Group, Calystus Wafula alisema presha ya pamoja kutoka kwa Azimio, mashirika ya kijamii na Wakenya kwa ujumla ndio itakayokomesha dhuluma za serikali ya Kenya Kwanza.

“Hii ndio maana tunatoa wito kwa mashirika ya kijamii kama vile Tume ya Kutetea Haki ya Kibinadamu (KHRC), Linda Ugatuzi, Kenya Bora Tuitakayo miongoni mwa mengine, kuungana na Azimio mnamo Ijumaa kule Kamukunji kutetea Wakenya wanaoumizwa na ushuru wa juu unaotozwa na serikali ya Ruto. Aidha, tunawaomba Wakenya wote kuweka kando miegemeo yao ya kisiasa na kupinga Sheria dhalimu ya Fedha,” akasema Bw Wafula.

“Saba Saba ni siku ya kihistoria ya kukumbuka mapambano ya kupigania kurejelewa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi na ukombozi wa pili. Wakati huu tunapigania ukombozi wa kiuchumi na kiutawala,” akaongeza huku akitaja kauli mbiu ya Kenya Kwanya, nyakati za kampeni ‘Pesa Mfukoni’ kama hadaa kwa mahasla.

Bw Wafula alisema ajenda ya mkutano wa Ijumaa haifaidi Bw Odinga, Martha Karua, Kalonzo Musyoka au viongozi wengine wa upinzani bali inahusu masilahi ya Wakenya wote.

Taarifa hiyo ya Jay Network Kenya pia ilitiwa saini na Katibu Mkuu Annie Thuku na Katibu Mkuu Albert  Kavita.

Wakati huo huo, Bw Odinga mnamo Jumanne alitangaza kuwa kando na mkutano wa Kamukunji, mikutano mingine sambamba itafanywa siku hiyo kote nchini kupigania kile alichokitaja kama ukombozi wa tatu dhidi ya utawala ‘dhalimu’ wa Kenya Kwanza.

“Kwa hivyo, tuko hapa kuwathibitishia Wakenya kuwa, mkutano wetu wa Kamukunji, Nairobi utafanyika Ijumaa jinsi tulivyotangaza awali. Lakini sio tu Kamukunji jijini Nairobi bali Kamukunji kote nchini ambako ukombozi huu wa tatu utazinduliwa,” akasema Jumanne kwenye kikao na wanahabari katika afisi za SKM Centre, Karen, Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Wapo wadudu wanaotumia kinyesi cha ndovu,...

Nauli ghali tena Wakenya wakiendelea kupambana na maisha

T L