• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Dennis Waweru atangaza mchakato wa BBI kutamatishwa kabla ya Agosti

Dennis Waweru atangaza mchakato wa BBI kutamatishwa kabla ya Agosti

Na MWANGI MUIRURI

MWENYEKITI Mwenza katika sekritarieti ya kufanikisha mchakato wa kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) nchini Bw Dennis Waweru amesema Jumatano kuwa referenda ni kabla ya Agosti.

Amesema kuwa “hakuna cha kutuzuia na kila msukumo kwa sasa ni kwamba mabunge ya Seneti na lile la kitaifa yatajadili mswada wa BBI kabla ya Ijumaa wiki ijayo na refarenda iandaliwe.

Akiwa katika mahojiano na runinga ya Inooro, Bw Waweru alisema kuwa Wakenya wanafaa kujiandaa kwenda kwa uchaguzi wa 2022 kukiwa na Katiba iliyofanyiwa marekebisho “na hilo litafanyika.”

Hali hii imeibua hisia, wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wakisema Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wameingia katika mfumo wa kiimla wa kugeuza mchakato wa BBI kutoka kwa maamuzi ya hiari hadi kwa msukumo wa “utapita mpende msipende”.

Mwinjilisti na mtunzi wa nyimbo za kumtukuza Mungu Bw Reuben Kigame, Jumanne aliambia Taifa Leo kuwa “hata sisi katika imani ya dini tumeshangazwa sana na hatua ya wawili hao kusema wanatuunganisha kwa masharti yao wenyewe bila kuzingatia maoni yetu kama Wakenya.”

Bw Kigame alisema wanaomba Mungu awape viongozi hao wawili busara ya kuwasikiliza wengine na kuelewa kuwa “masuala ya kuongoza watu 47 milioni hayawezi yakaafikiwa na wao wawili tu na kisha kutaka msimamo wao uidhinishwe kwa nguvu.”

Bw Kigame aliwataka Wakenya wote walio na maono pana ya kuhitaji kuheshimiwa na viongozi wao katika kufamya maamuzi ya kiutawala wazame kwa maombi ya kumlilia Mungu awanusuru kutoka kwa “uongozi ambao umepoteza mwelekeo na usiojali msingi wa kikatiba ambao unawapa wananchi kipaumbele katika kujiamlia jinsi ambavyo wangetaka kutawaliwa.”

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Ngugi Njoroge alisema kuwa “huu ni wakati mgumu sana kwa historia ya taifa hili.”

“Wagonjwa na wanaoandamwa na kuadimika kwa chanjo ya Covid-19 na oksijeni hospitalini huku pia wakikosa uhakika wa usalama wao, serikali yenyewe ikiwaambia zaidi ya 1.5 Milioni watakumbwa na njaa kabla ya Agosti, kuhitajika tena kutumia mabilioni kuingia kwa refarenda ambayo nia kuu hata haijulikani na Wakenya wengi,” akasikitika Prof Njoroge.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata alisema kuwa BBI kwa sasa imegeuzwa kuwa chanjo ya maradhi ya kisiasa ambayo hakuna anayeyaelewa, huku taifa likiumia chini ya madeni kupindukia, mahangaiko ya njaa na vifo kutokana na Covid-19.

“Kando na Covid-19, sasa tumekumbwa na mkurupuko mwingine wa BBI ambapo tunaambiwa lazima tumeze refarenda kama chanjo. Lengo kuu la BBI nchini hata halieleweki na mwelekeo wa mwisho unaonekana ni Rais na Bw Odinga wanalenga kujipa mpangilio wa kuunda mirengo yao ya uwaniaji urithi wa 2022,” akasema seneta Kang’ata.

Bw Kang’ata alisema kuwa anatazamia hali kwamba mrengo wa Kieleweke unalenga kutumia nyadhifa zinazopaniwa kuongezewa na BBI kuunda mpangilio wa serikali ya kuongozwa na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi akiwa na Peter Kenneth kama Naibu wake huku Bw Gideon Moi akikabidhiwa Uwaziri Mkuu.

Alisema kuwa hesabu ya Kieleweke ni kwamba, BBI ndiyo tu inayoweza kuwapa nyadhifa za kuwasaidia kuwatenga Bw Odinga na Naibu wa rais Dkt William Ruto ili muundo wao wa uwaniaji ujipe mashiko.

“Kwa upande wake, Bw Odinga anasukumana apate kitu cha kuhadaa wafuasi wake kuhusu uamuzi wake wa kuingia Kanani Machi 2018 akiwa peke yake na kuwaacha wafuasi wake katika kingo za Mto Jordan. Anataka azindue kampeni zake za 2022 kwa msingi kuwa daraja aliyokuwa ameenda kujenga sasa imekamilika na amewarejelea wafuasi wake sasa akawavukishe salama hadi Kanani,” asema.

Anasema kuwa BBI imegeuzwa sasa kuwa mradi wa kibinafsi wa hao wawili wa kusaka malengo yao ya urithi wa 2022 wala sio kwa manufaa ya Wakenya wote.

Anayeongoza vuguvugu la Linda Katiba akipinga BBI, Bi Martha Karua anasema kuwa “ule utundu na utukutu wote ambao tumekuwa tukitahadharisha Wakenya kuhusu BBI ndio sasa unajitokeza wazi.”

Bi Karua alisema kuwa BBI haukuwa mradi wa Wakenya kwa kuwa “mapendekezo yao katika mkila jukwaa yamekuwa maisha yao yaboreshwe, nafasi za ajira ziundwe kwa vijana, mzigo wa ushuru uteremke na gharama za mishahara kwa mashirika, taasisi na muundo wa serikali iteremke.”

Anasema nayo BBI ililetwa kwa msingi wa kuongeza madeni ya kitaifa, kupandisha zaidi mzigo wa mishahara kupitia kupanua serikali na pia kupenyeza siasa za mapendeleo ambapo wandani na marafiki wa vinara hao wawili wa BBI wanalenga kuwatuza katika serikali ijayo.

Alisema kuwa BBI kwa sasa imedhihirika kuwa sio mpango wa kuunganisha Wakenya bali ni wa kuunganisha vinara wa kikabila kwa nia ya kutwaa serikali 2022.

“Hiyo ndiyo hali ambayo sasa tunafaa kukasirikia kama taifa na kwa pamoja tukatae kuidhinisha njama hiyo. Pesa za umma zimetumiwa vibaya sana hapa nchini kusukuma mpango wa kuthibiti urafiki wa kifamilia. Rais Kenyatta analenga tu masilahi yake ya kufungia wengine nje ya usawa wa kuwania urais 2022 huku Bw Odinga akiwa na malengo sawa na hayo. Kinachoibuka kama sarakasi sasa ni kuwa, Rais analenga BBI iwe silaha yake dhidi ya Bw Odinga na Naibu wa Rais Dkt William Ruto,” asema.

Pia, kwa upande wake, akaongeza, Bw Odinga akilenga BBI iwe silaha yake dhidi ya Rais na pia Dkt Ruto “hivyo basi kudunisha maamuzi Sya kutumia mabilioni ya pesa kuandaa mradi tu wa kujinufaisha wenyewe, sisi wengine wote tukiachwa kupambana na taharuki za ugonjwa wa Covid-19, mfumko wa bei na umasikini unaotokana na kupotea kwa ajira na biashara kuporomoka.”

You can share this post!

Watford wahitaji alama nne pekee kutokana na mechi tatu...

‘Nahisi upweke licha ya kuwa kwenye ndoa’