• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Jamii ya Watta yalia kuishi Kenya kabla ipate uhuru na haijatambuliwa kuwa kabila

Jamii ya Watta yalia kuishi Kenya kabla ipate uhuru na haijatambuliwa kuwa kabila

Na ALEX KALAMA

HUKU Taifa la Kenya likijivunia miaka 58 tangu lipate uhuru wake kutoka kwa wakoloni, jamii ya Watta wanaoishi katika Kaunti ya Kilifi imesema haijaona faida yoyote ya kujivunia uhuru huo.

Licha ya kuishi humu nchini kwa miaka mingi hata kabla ya Kenya kupata uhuru hadi sasa, bado hawajatambulika rasmi na serikali kama mojawapo ya makabila ya taifa la Kenya.Watta ni jamii ya watu wanaoorodheshwa katika kundi la Wakushi wanaoaminika kuwa na chimbuko lao katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Ni jamii ambayo inaamini kutambulika hata katika vitabu vya dini ambavyo vinaeleza kuwa mke wa Nabii Musa alitokea katika jamii hiyo ya wakushi.Inasemekana kuwa, katika safari yao ya kuja nchini Kenya kutoka Mashariki ya Kati, Wawatta walipitia Bahari ya Shamu na kuingia nchini Misri, kisha wakafika nchini Uhabeshi, ambako walijigawa makundi mawili.

Kundi moja lilisalia nchini Uhabeshi, na jingine likaelekea nchini Kenya kupitia kusini ya Uhabeshi.Jamii hiyo baada ya kuingia nchini Kenya inadaiwa kujigawa makundi mawili, ambapo kundi la kwanza liliekea Isiolo na Marsabit katika eneo la Mashariki ya Kenya, japo wanadaiwa kufanana sana na watu wa jamii ya Borana.

Kundi la pili likielekea mkoa wa Pwani na kupata makazi katika maeneo ya Garsen, Hola, Tarasaa, Ege Kumbi, na Bilisa katika Kaunti ya Tana River, huku wengine wakipata makazi yao huko Chamari, Kasikini, Gongoni, Dabaso, Roka, Bamba, Jila, Shirango katika Kaunti ya Kilifi.

Wengine wao walijitafutia makazi karibu na ufuo wa Bahari Hindi katika Kaunti ya Kilifi, huku wengine wakipata makazi yao katika Kaunti za Taita Taveta na eneo la Samburu, Kaunti ya Kwale.Jamii ya Watta inafahamika kwa shughuli za uwindaji na ulaji nyama.

Vile vile, ni jamii ya kuhamahama na hivyo ndivyo wengine wao walifanikiwa kuingia hata taifa jirani la Tanzania.Wawatta wamekuwa wakibadilishwa majina na jamii zinazowakaribisha katika makazi yao; jamii ya Wagiriama ikiwaita Waryangulo, Waswahili wakiwaita Wasanya na huko nchini Tanzania wakiitwa Wadegere, neno hili likimaanisha “umeona”.

Kulingana na mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii hiyo ya Watta, Bw Onoto Jilo, jamii ya Watta ina mbari 12. Hizo ni; Hajejeh, Guluh, Kaararah, Maamboye, Suunkanah, Gaamadoh, Meetah, Kujeegah, Ilaanih, Maandoyo, Waayuh na Jaalantuh.Anasema uchumi wa jamii ya Watta ulisambaratika baada ya serikali kupiga marufuku uwindaji.

“Uchumi wa jamii ya Watta ulitegemea uwindaji. Hatukujua mambo ya ukulima. Tulikuwa na mazoea kuwinda na kula nyama pamoja na maisha ya kuhamahama,” alisema Bw Jilo.Kwa muda mrefu jamii ya Watta haijazingatia elimu kutokana na kuhamahama kila wakati na kuendeleza shughuli ya kutafuta ulaji kwenye misitu ya Tsavo miongoni mwa misitu mingine.

Kutokana na adhabu kali iliyopewa waliokiuka amri ya kutowinda, wengi waliamua kutoroka maeneo yaliyokuwa karibu na shule. Hii ilisababisha wengi kukosa elimu hata baada ya Kenya kupata uhuru wake. Kukosa eli,u ya kutosha pia kumechangia watu wa jamii ya Watta, kutokuwa na sauti katika masuala ya siasa.Hii ni licha ya katiba ya taifa la Kenya kueleza kuwa jamii ndogo pia ziweze kuwakilishwa.

“Kinachotushangaza ni kwamba licha ya jamii yetu kuja Kenya hata kabla ya taifa hili kupata uhuru. Hadi sasa bado hatujapewa kodi ya kuonyesha kuwa sisi ni Wakenya. Hali hii imechangia jamii yetu kusalia nyuma sana kimaendeleo na vile vile kutengwa katika uwakilishaji.

“Licha ya katiba ya taifa hili kueleza kuwa hata jamii ndogo zinafaa kuwakilishwa, hilo hatujaliona likifanyika kwetu. Hata kunapotokea nafasi utaona kuwa nafasi zile bado zinapewa jamii nyingine na sisi tunaachwa hivyo,” alisema Bw Jilo.Mwenyekiti huyo anatoa wito kwa serikali kuitambua jamii hiyo kwa angalau yale masuala muhimu, kama vile vijana kupewa ajira, wanafunzi kupewa pesa za basari ili waweze kuendelea na masomo.

Bw Jilo ambaye alikuwa mmoja wa wawakilishi wakati wa Kongamano la Katiba huko Bomas of Kenya anadai aliunga mkono kifungu cha 56 cha katiba mpya ambacho kinazungumzia uwakilishi sawa na anahimiza kifungu hicho kitekelezwe ipasvyo.

“Kifungu cha 56 cha katiba ya Kenya kinaeleza wazi kuwa kila jamii inafaa iwakilishwe sawa ila kwa sasa jambo hilo halijawahi kutekelezwa kwa jamii yetu ya Watta. Naiomba serikali itekeleze agizo la kifungu hiki cha katiba ili hata jamii yetu iweze kunufaika,” alisema Bw Jilo.

Analia kuwa japo serikali inasema imeipa jamii hiyo nambari ya usajili kama kabila la 45 Kenya, bado jamii hiyo haijatambuliwa kikamilifu na serikali kwani nambari hiyo baadaye ilipewa jamii ya Washona.

You can share this post!

2022: Mudavadi akataa Huduma Namba katika uchaguzi

Elgon Kenya na UoN kushirikiana kuanzisha mafunzo ya...

T L