• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
2022: Mudavadi akataa Huduma Namba katika uchaguzi

2022: Mudavadi akataa Huduma Namba katika uchaguzi

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi amepinga vikali matumizi ya Huduma Namba kutayarisha sajili ya wapigakura akisema ni njama ya kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mswada wa Huduma Namba uliowasilishwa Bungeni unapendekeza itumiwe kutayarisha sajili ya wapigakura. Ukipitishwa kuwa sheria, unaweza kuathiri maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao. Bw Mudavadi alisema kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haifai kuelekezwa data inayopaswa kutumia kutayarisha sajili ya wapigakura kwa kuwa ina data kuhusu uchaguzi inazopaswa kutumia.

“IEBC ndiyo mhifadhi wa data za wapiga kura na sajili ya wapigakura na matumizi ya mfumo wa Huduma Namba yataathiri vibaya jukumu lake na kuonekana kama kuna IEBC nyingine,” alisema. Kulingana na kinara mwenza huyo wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA), matumizi ya Huduma Namba yatahujumu maandalizi ya uchaguzi huru na wa haki.

“Kwa wakati huu wengi nchini Kenya wanakubaliana kwamba tuko na ukosefu mkubwa wa kuaminia na hicho ni kiungo muhimu cha uchaguzi utakaozua migawanyiko ambao nchi imekuwa ikipitia,” alisema kwenye taarifa aliyotumia vyombo vya habari jana.

Alisema IEBC ikiwa tume huru, haiwezi kuwa na Afisa Mkuu Mtendaji wake akiketi katika bodi ya Huduma Namba “ kwa kuwa hii inahujumu uhuru wake na kuzua mgongano wa maslahi.” “Huduma Namba ilihusu kusajiliwa kwa watoto ambao hawaruhusiwi kupiga kura,” alieleza Bw Mudavadi. Ikiwa huduma namba itatumiwa katika kuandaa sajili ya wapigakura, aeleza, kuna hatari ya raia wengi kukosa kupiga kura.

Vile vile, alisema hatua hiyo itavuruga maandalizi ya sajili ya wapigakura kwa vile IEBC imepiga hatua. “IEBC iko katika mchakato wa kukamilisha ukaguzi wa sajili ya wapigakura na kuanzishwa kwa huduma namba kutayarisha sajili hiyo kutakuwa na athari hasi kwa mchakato huo na kuhujumu maandalizi ya tume ya kuandaa uchaguzi huru na wa haki,” alisema.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema kwamba hatua ya kutumia huduma namba kutayarisha sajili ya wapigakura inaweza kuwa njama ya serikali kuu kuteka nguvu za IEBC za kusimamia uchaguzi.

Bw Mudavadi alikumbusha Wakenya kwamba mchakato wa kusajili Wakenya kwa huduma namba ulipingwa kortini na Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu na mashirika mengine yasiyo ya serikali na kijamii na Kenya Human Rights Commission na Nubian Rights Forum yaliyolalamikia ukosefu wa sera na sheria ya ulinzi wa data.

Mahakama Kuu ilikubaliana na walalamishi na kuagiza serikali kutatua suala la usalama wa data za watu binafsi kabla ya mradi wa Huduma Namba kuendelea. “Huduma Namba ina mapengo makubwa yanayoifanya kutoaminiwa na umma. Haifai kutumiwa kutayarisha sajili ya wapigakura ya uchaguzi wetu mkuu ujao,” alisema Bw Mudavadi.

Anasema uamuzi wa korti kwamba mchakato unaostahili unapaswa kufuatwa ili umma uweze kuwa na imani na Huduma Namba.

You can share this post!

Kinaya cha UDA kuponda familia ya gavana Joho

Jamii ya Watta yalia kuishi Kenya kabla ipate uhuru na...

T L