• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Salman taabani kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi

Salman taabani kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi

Na MARY WANGARI

KARLSRUHE, Ujerumani

SHIRIKA la Kimataifa la Vyombo vya Habari, limewasilisha kesi ya uhalifu katika korti ya Ujerumani dhidi ya Mwanamfalme Mohammed bin Salman na maafisa wengine wakuu wanne.

Shirika hilo la Wanahabari Wasio na Mpaka (RSF) limewasilisha mashtaka ya “uhalifu dhidi ya binadamu” kuhusiana na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Tangazo kuhusu kesi ya shirika hilo lilijiri Jumanne, Machi 2, siku nne baada ya Amerika kutoa ripoti wazi ya ujasusi.

Ripoti hiyo ilifichua kuwa mwanamfalme almaarufu kama MBS, aliidhinisha mauaji ya mwanahabari huyo wa Saudi Arabia.

Khashoggi, alikuwa mwandishi wa makala katika gazeti la Washington Post na mkosoaji sugu wa sera za Saudi chini ya utawala wa mwanamfalme.

Aliuawa katika Ubalozi wa Saudi, jijini Istanbul mnamo Oktoba 2018.

Mauaji hayo ya kinyama yaliyoongozwa na kitengo cha walengaji shabaha cha Saudi yalivutia hisia kali kote duniani na kuathiri vibaya hadhi ya MBS ulimwenguni.

Kesi hiyo, inayoomba uchunguzi kufanywa na waendeshaji mashtaka chini ya sheria za kimataifa za Ujerumani, inaishutumu Saudi Arabia dhidi ya kumdhulumu Khashoggi pamoja na wanahabari wengine kadhaa.

“Tunamhimiza mwendeshaji mashtaka Ujerumani kutangaza msimamo,”

“Hakuna mtu anayepaswa kuwa juu ya sheria ya kimataifa, hasa wakati hatia dhidi ya utu zimo hatarini,” alisema Katibu Mkuu RSF, Christophe Deloire, kupitia taarifa.

Baada ya ripoti hiyo kutolewa, mchumba wake Khashoggi’s alitoa wito kwa MBS kuadhibiwa “bila kucheleweshwa.”

Utawala wa Rais wa Amerika Joe Biden umeamua kutoweka vikwazo dhidi ya mwanamfalme wa Saudi kwa mauaji ya Khashoggi.

Maafisa wa Saudi walikanusha ripoti hiyo wakisisitiza kuwa Khashoggi aliuawa katika “oparesheni ya uhuni” ambayo haikumshirikisha mwanamfalme – ambaye ni kiongozi wa kimabavu wa ufalme huo.

Hata hivyo, RSF ilisema imekusanya ushahidi kuhusu “sera ya utawala ya kuwashambulia na kuwanyamazisha wanahabari” ambao iliwasilisha kwa Mahakama ya Umma, mjini Karlsruhe, Ujerumani, mnamo Jumatatu, Machi 1, 2021.

Ripoti yake imesimulia kwa kina visa vya wanahabari wengine 34 waliofungwa jela nchini Saudi Arabia, akiwemo bloga Raif Badawi, ambaye amefungwa gerezani tangu 2012 kwa mashtaka ya “kutukana Uislamu”.

You can share this post!

Austria, Denmark zavunja uhusiano kuhusu chanjo ya corona

Mihemuko kuhusu video ya utani Pakistan