• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Mtangazaji Amina Abdi awatolea kucha wanaomsuta kwa kumtetea DJ Joe Mfalme

Mtangazaji Amina Abdi awatolea kucha wanaomsuta kwa kumtetea DJ Joe Mfalme

NA SINDA MATIKO

MTANGAZAJI staa Amina Abdi kawatolea kucha wanaomsuta kwa kumtetea DJ Joe Mfalme ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya polisi.

Bw Joseph Mwenda Munoru almaarufu DJ Joe Mfalme kajikuta kakalia kuti kavu baada yake kuburuzwa kwenye kesi ya mauaji ya afisa wa polisi Felix Kitosi.

Inadaiwa kuwa mburudishaji huyo na wapambe wake walimvamia kwa ngumi Kitosi kwenye mtafaruku uliozuka baada yake kuligonga gari la DJ Joe Mfalme.

Kando na DJ Joe Mfalme, pia wametiwa mbaroni maafisa polisi watatu wanaodaiwa kumshambulia vile vile Kitosi alipoambatana na mburudishaji huyo hadi kituo cha polisi kuenda kuandikisha taarifa ya kisa hicho. Kitosi alifariki siku sita baada ya kushambuliwa.

Na huku uchunguzi ukiwa unaendelea, Amina ambaye amefanya kazi siku nyingi na DJ Joe Mfalme kiasi cha kuishia kuwa wandani wa karibu sana, juzi kati alijitokeza hadharani kwenye mitandao ya kijamii kumtetea DJ Joe, akisistiza kuwa msela hakuhusika katika kumshambulia Kitosi.

Ni kauli iliyowakoroga nyongo baadhi ya watu walioanza kumshambulia kwa kumtetea swahiba wake wakati uchunguzi ukiwa ndio umeanza.

Lakini Amina anasema hatatereshwi.

“Wala hainisumbui… chuki za mitandaoni… labda waje na jipya. Nimeishi kuchukiwa… kwa hilo sioni kipya kwenye hilo wala hainisumbui wanaonishambulia,” Amina anasema.

Huku akisisitiza kwamba ana imani kubwa kuwa mwisho wa siku DJ Joe atakuja kuachiliwa huru.

“Kila mja anaye mtu wake ambaye anaweza kusimama na kumtetea kindakindaki. Kama unamfahamu DJ Joe Mfalme kama mimi ambaye nimemfahamu kwa miaka mingi, basi utakuwa unajua ni mtu mngwana sana, mkarimu na mstaarabu mwenye kuipenda kazi yake na asiyependa vurugu. Joe wala hatumii dawa za kulevya wala kileo chochote kwa hiyo, huwezi kuniambia kisa hicho kilipotokea labda alikuwa kalewa na huenda alifanya jambo,” anasema Amina.

Kwa wanaomsuta kwa kumtetea Joe pasi na kujali familia ya waliofiwa, Amina anayo kauli.

“Ndio ni kesi ngumu maana yametokea mauaji na familia ya waliofiwa tunawaombea nguvu na utulivu lakini mimi nitasimama pale pale, Joe sio mtu wa hivyo na wala simzungumzi mtu mwingine maana wapo wengine walioshtakiwa naye… Nasema huyu Joe ninayemjua mimi, wala hakuhusika kwenye kumshambulia afisa huyo,” akatiririza.

Aidha Amina anasisitiza kuwa anaelewa ni kwa nini baadhi ya mastaa ambao ni watu wa karibu wa DJ Joe Mfalme hawajajitokeza kuonyesha sapoti yao hadharani kama yeye.

“Naelewa kutokana na uzito wa jambo hilo labda pengine watu wake wengine wa karibu wanahofia kuizungumzia ishu hiyo mitandaoni au kujitokeza mahakamani kumsapoti. Lakini urafiki ni nini kama sio kusimama na swahiba wako hata pale anapokuwa na majanga?” amehoji.

Kwa sasa DJ Joe Mfalme atazidi kusotea nyuma ya nondo baada ya Hakimu Mwandamizi Margaret Murage kuamuru kwamba washukiwa wote wazuiliwe kwa siku 14 ili kupisha maafisa wa usalama kukamilisha uchunguzi wao kwenye mauaji hayo.

Awali maafisa wa upepelezi walikuwa wameiomba mahakama siku 21 lakini Hakimu Murage akatupilia mbali ombi hilo kwa msisitizo kuwa siku 14 zinatosha.

Kutokana na amrisho hilo, DJ Joe Mfalme sasa atalazimika kuingia hasara kubwa ya shoo alizokuwa ameratibiwa kufanya kwenye sikukuu za Pasaka zinazokaribia.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume akejeliwa kwa kuruhusu mkewe kupanga uzazi

Murang’a yapiga marufuku disko matanga, vileo wakati wa...

T L