JAMVI: Njama ya Raila kubomoa One Kenya Alliance

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Raila Odinga, ameanza mikakati ya kuwapiga vita vya kisiasa vinara wenza katika National Super Alliamce (NASA), muungano aliotumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, ambao wameungana chini ya muungano wa One Kenya Alliance.

Mikakati yake inahusisha kubomoa muungano wa One Kenya Alliance ambao unashirikisha kiongozi wa chama cha Wiper Stephen Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu hata kabla haujatamba.

Katika juhudi zake za kuubomoa muungano huo, Bw Odinga ameanza kumshawishi Bw Moi kujiunga naye katika hatua za kuwatenga Bw Musyoka, Bw Musalia na Bw Wetangula ambao ni washirika wake katika NASA.

Watatu hao walimtenga Bw Odinga wakidai alisaliti mkataba wa NASA kuhusu ugawaji wa mapato na nyadhifa bungeni pamoja na kuunga mmoja wao kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Mapema wiki hii, Bw Odinga alikutana na Bw Moi na Bw Muhoho Kenyatta ambaye ni kaka mdogo wa Rais Uhuru Kenyatta katika kile ambacho wadadisi wa siasa wanasema ni mipango yake ya kuwatenga Musyoka, Mudavadi na Wetangula.

Bw Moi ana uhusiano wa karibu na Rais Kenyatta, kinara mwenza wa Bw Odinga katika handisheki. Inasemekana Muhoho ni mmoja wa washauri wa kaka yake mkubwa Rais Kenyatta.

Ingawa Muhoho hajawahi kuhusika moja kwa moja na siasa, wadadisi wanasema ni mmoja wa wanaotekeleza jukumu muhimu kupanga siasa za urithi baada ya kaka yake kustaafu 2022. Tangu handisheki amekuwa akimchangamkia Bw Odinga.

Duru za kisiasa zimekuwa zikidai kwamba Rais Kenyatta anapendelea muungano wa One Kenya Alliance jambo ambalo limezua minong’ono katika ODM kwamba anamsaliti Bw Odinga baada ya kumsaidia kumzima naibu wake William Ruto kupitia handisheki.

Dalili zinaonyesha kuwa Bw Odinga anavuruga ngome za Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula ili kuwanyima umaarufu waliofurahia baada ya chaguzi ndogo za hivi majuzi ambazo waliungana kubwaga ODM.

Katika ngome ya Bw Musyoka ya Ukambani, amemvuta Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana upande wake. Kivutha ni hasimu wa kisiasa wa Bw Musyoka ambaye pia ametangaza azma ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mnamo Jumanne, Bw Odinga alituma ujumbe wa maafisa wa chama cha ODM kukutana na Profesa Kibwana kujadili uwezekano wa wawili hao kushirikiana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Ujumbe huo ulioshirikisha maafisa wa ODM kutoka kaunti za Ukambani Makueni, Kitui na Machakos ulisema kwamba ulimrai Gavana Kibwana kushirikiana na Bw Odinga.

Katika ishara kwamba aliunga hatua ya Bw Odinga ya kumzima Bw Musyoka, Profesa Kibwana alimtaka waziri huyo mkuu wa zamani pia kuzungumza na mwenzake wa Machakos Alfred Mutua na Charity Ngilu wa Kitui.

Alifichua kwamba alikuwa amezungumzia suala la kubuni muungano wa kisiasa na Bw Odinga walipokutana mapema mwaka huu.

Bw Kibwana na Bw Mutua wanaohudumu kipindi chao cha mwisho cha ugavana ni wakosoaji wakubwa wa Bw Musyoka.

Katika eneo la Magharibi ambalo ni ngome ya kisiasa ya Bw Mudavadi na Bw Wetangula, Bw Odinga amemrai aliyekuwa katibu wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu biashara Mukhisa Kituyi kumuunga mkono.

Mnamo Februari, Bw Odinga alikutana na Dkt Kituyi na Gavana Kibwana na tangu wakati huo, minong’ono ya kuungana nao ilianza kushika kasi.

Dkt Kituyi anatoka Bungoma anakotoka Bw Wetangula na inasemekana Bw Odinga anawarushia chambo wanasiasa wengine wa kaunti hiyo.

Katika eneo la Magharibi, Bw Odinga ameimarisha usuhuba wake na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na inasemekana amekuwa akiwarushia chambo wanasiasa wengine wa eneo hilo walio na ushawishi mkubwa mashinani.

Wandani wa Bw Odinga wanasema kwamba ameanza njama ya kuhakikisha kuwa Rais Kenyatta amebadilisha nia ya kuunga One Kenya Alliance kwa kuvuta Bw Moi upande wake.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanasema kwamba hii inatokana na tetesi kwamba washirika wa karibu wa rais wanataka Bw Moi kumrithi.

“Akifaulu kubomoa One Kenya Alliance kwa kuukosesha uungwaji mkono na Rais Kenyatta basi Bw Odinga atakuwa ameondoa kisiki katika azima yake ya kuingia ikulu. Hii haimaanishi itakuwa mteremko kwake hata akiungwa na Rais Kenyatta mwenyewe kwa sababu vinara wa One Kenya Alliance wanaweza kuungana na Naibu Rais Ruto na kumtoa jasho kwenye kampeni,” asema mdadisi wa siasa Lawrence Koech.

Mdadisi huyu anasema kwamba hatua ya Bw Odinga kumrai Bw Moi, inaonyesha kuwa hayuko makini kuungana na Dkt Ruto ilivyodaiwa.

Uwezekano wa Bw Odinga na Dkt Ruto kuungana uliibuka naibu rais alipokutana na Gavana Oparanya kaunti ya Narok wiki jana ambapo inasemekana walijadili siasa za urithi za 2022.

“Bw Odinga anataka kucheza pande zote na nia yake kuu ni kuvuruga mipango ya vinara wenza katika NASA ili wasiungwe mkono na Rais Kenyatta au kuungana na Dkt Ruto,” aeleza Koech.

One Kenya Alliance ina mchongoma wa kupanda kisiasa

Na WANDERI KAMAU

WAANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta wanakabiliwa na kibarua kigumu kuujenga muungano wa One Kenya Alliance, kwa kuvuruga uungwaji mkono wa Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika ngome zao.

Juhudi hizo ziliibuka wiki iliyopita, ilipobainika kwamba kumekuwa na njama fiche ambazo zimekuwa zikiendeshwa na maafisa wakuu katika Ikulu kufadhili shughuli za muungano huo.

Muungano huo unawashirikisha kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Chama cha ODM kimekuwa kikilalamikia “kupendelewa” kwa muungano huo na serikali, hasa baada yake kuibuka mshindi kwenye chaguzi ndogo za maeneobunge ya Matungu, Kabuchai na Kaunti ya Machakos.

Kufichuka kwa njama hizo ndiko kunakotajwa kuchangia Rais Kenyatta kumwendea kwa haraka Bw Odinga mnamo Jumatano, ili kuzima wasiwasi ambao ulikuwa umeibuka kuhusu handisheki na mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta alifanya kikao cha faragha na Bw Odinga katika makazi yake mtaani Karen, jijini Nairobi, ili kujaribu kumhakikishia kuwa kila kitu ki shwari.

“Rais Kenyatta alimhakikishia Bw Odinga kuwa kila kitu ki shwari,” zikaeleza duru.Licha ya mkutano huo, imeibuka kwamba huenda ikawa kibarua kigumu kwa wandani wa Rais Kenyatta kuujenga muungano huo, hasa ikiwa lengo lao ni kuvuruga ufuasi wa Dkt Ruto na Bw Odinga katika ngome zao.

Wadadisi wa siasa wanasema licha ya muungano huo kupata ushindi kwenye chaguzi ndogo kadhaa zilizopita, Dkt Ruto na Bw Odinga bado ni wanasiasa wenye ushawishi na ufuasi mkubwa sana katika ngome zao.

Vile vile, wanaeleza kwamba huenda njama hizo zikaimarisha uungwaji mkono wao miongoni mwa wafuasi wao, ikiwa itabainika kuwa lengo la muungano huo ni kuwaingilia kisiasa.

“Dkt Ruto na Bw Odinga ni viongozi ambao wana wafuasi wanaowaamini na kuwategemea sana. Ni wanasiasa wenye uwezo wa kuwaagiza wafuasi wao kufuata mwelekeo wowote wa kisiasa. Hivyo basi, ikiwa itabainika kwamba lengo la muungano wa One Kenya Alliance ni kuwaingilia, basi hilo huenda likawajenga hata zaidi,” akasema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kwa mujibu wa mikakati ya wandani hao wa Rais, wanalenga kupunguza umaarufu wa Bw Odinga katika ukanda wa Pwani na eneo la Kisii, ili kumsawiri kama kiongozi wa eneo la Luo Nyanza pekee.

Inaelezwa kuwa katika ukanda wa Pwani, maafisa hao ndio wanaopanga mikakati ya kubuniwa kwa chama huru cha kisiasa, kwa kuwafadhili magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kilifi) na Amason Kingi (Kwale).

Duru zinaeleza kwamba ni kutokana na msukumo huo ambapo Gavana Kingi alisisitiza majuzi kuhusu haja ya eneo hilo kuwa na chama chake cha kisiasa mbele ya Bw Odinga.

Baadhi ya vyama vinavyopendekezwa kufufuliwa upya ni Shirikisho na Kaddu Asili.Kwenye msururu wa mikutano aliyofanya eneo la Pwani kabla ya kutangazwa kuambukizwa virusi vya corona majuma mawili yaliyopita, Bw Odinga alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Bw Kingi, aliyesisitiza kuwa wakati umefika kwa Wapwani kuwa na chama chao ambacho kitakuwa sauti yao katika ulingo wa kitaifa.

“Maeneo mengine nchini yana vyama vyao ambavyo huwasilisha maslahi yao katika meza ya kitaifa. Wakati umefika kwa Mpwani kuwa na jukwaa litakalokuwa kama sauti yake,” akasema Bw Kingi, huku akishangiliwa na wenyeji.

Kulingana na wadadisi, kibarua kingine kinachowakabili maafisa hao wenye ushawishi serikalini ni kupunguza umaarufu wa Dkt Ruto katika ukanda wa Bonde la Ufa.

Kufikia sasa, ukanda huo umegawanyika kati ya Dkt Ruto na Gideon ambapo wote wametangaza nia ya kuwania urais 2022.Hata hivyo, wadadisi wanasema licha ya kujitokeza kuanza kuvumisha azma yake, Gideon bado hajaonyesha makali ya kisiasa, ikilinganishwa na Dkt Ruto.

“Ilivyo sasa, Dkt Ruto bado anaonekana kuwa na udhibiti na usemi mkubwa wa kisiasa Bondeni ikilinganishwa na Gideon. Itawalazimu wandani hao wabuni mikakati mipya ya kumuuza Gideon kwa wananchi,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kando na hayo, kibarua kingine ni kupenya ukanda wa Mlima Kenya, ambako ni ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta.Wadadisi wanasema kwamba ilivyo sasa, eneo hilo limegawanyika mara mbili —kati ya wale wanaomuunga mkono Rais na wale wanaohisi amewasaliti, hasa kuhusu masuala ya kilimo.

Katika mazingira hayo, wanaeleza kwamba ni vigumu kwa muungano huo kupenya bila mwonekano wa Rais Kenyatta.

“Itabidi Rais Kenyatta ajitokeze mwenyewe kuunadi muungano huo kwa wananchi, ikiwa wanasiasa hao ndio anaowapendelea kuwa warithi wake. Hilo ndilo litakalouwezesha kupenya na kukubalika kisiasa katika eneo hilo. La sivyo, huenda juhudi hizo zikabaki kuwa kibarua kizito kwa wale wanaouendesha mchakato huo,” asema Bw Muga.

‘One Kenya Alliance haitegemei kumuondoa Raila kwa hesabu ya BBI’

Na SAMMY WAWERU

MUUNGANO mpya wa One Kenya Alliance haulengi kumuondoa yeyote katika mahesabu ya Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), amesema kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka.

Bw Kalonzo alisema muungano huo unaomjumuisha pamoja na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula (Ford-Kenya) na Gedion Moi (Moi) hauna nia ya kumuondoa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga katika mchakato wa BBI kama inavyodaiwa.

“Hakuna jaribio la kumuondoa yeyote katika mchakato wa BBI,” Kalonzo akasema.

“Tunaihitaji ODM na kiongozi wake, Bw Raila Odinga katika muungano wa One Kenya Alliance na unaolenga kuleta Wakenya pamoja na kuwaunganisha. Hatuna njama yoyote fiche,” akaelezea.

One Kenya Alliance ilizinduliwa siku kadha zilizopita, na baadhi ya wandani wa Bw Odinga, akiwemo mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed wamedai muungano huo una mkono wa serikali kumuondoa kiongozi wa ODM katika mahesabu ya BBI.

“Nitamtafuta huyo Junet aniambie shida iko wapi,” akasema Bw Kalonzo.

Huku Kenya ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu 2022, Kalonzo alisema miungano kadhaa ya kisiasa itabuniwa.

BBI ilizinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Raila Odinga, baada ya kufanya salamu za maridhiano, maarufu kama Handisheki.