• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Utawala wa Moi ulitesa Pwani, Joho aambiwa

Utawala wa Moi ulitesa Pwani, Joho aambiwa

Na KAZUNGU SAMUEL

ZIARA ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho hadi nyumbani kwa Rais Mstaafu Daniel Moi, huko Kabarak wiki iliyopita inaendelea kuleta hisia mseto za kisiasa Pwani.

Baadhi ya wabunge walioongea na Taifa Jumapili walisema kuwa utawala wa Rais Moi ulitesa sana wakazi wa Pwani.

Kwa sababu hiyo, walisema ziara ya Joho huenda ikamfanya akapoteze umaarufu na kisha kukosa kuungwa mkono katika eneo la Pwani.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Bw Owen Baya alisema kuwa Gavana Joho bado hajapatiwa idhini na watu wa Pwani kufanya kazi na Gedion Moi.

“Wasiwasi wangu ni kuwa huenda Gavana Joho anajaribu kusukuma eneo la Pwani katika ukuta usio na matumaini akisingizia kuunganisha wakenya.

Kwa yeye kusema kwamba anataka umoja wa taifa la Kenya, angefaa kuanza na umoja wa Pwani.

“Kabla ya kuelekea na kurekebisha mlango wa jirani, anza kwa kurekebisha kwako,” akasema Bw Baya.

Mbunge huyo alisema kuwa ingawa kila mkenya ana haki ya kutembela mtu yeyote nchini na kumjulia hali, mkazi wa Pwani kumtembelea Moi kwa ajili ya kisiasa vinatoa sura isiyopendeza,” akasema Bw Baya.

Maoni yake yaliungwa mkono na mbunge wa Magarini Bw Michael Kingi ambaye alisema kuwa ukanda wa Pwani ulipata shida chini ya utawala wa Rais huyo mstaafu.

“Tulitaabika sana Pwani na tutaunga mkono azimio la Joho kama lengo lake lilikuwa ni kutafuta uungwaji mkono wala sio yeye akaunge mkono familia ya Moi irudi uongozini tena,” akasema mbunge huyo.

Naye mbunge wa Kisauni Bw Ali Mbogo alisema kuwa hatua ya Gavana Joho ilikuwa sawa kwa vile itatoa fursa kwa Pwani kuwa katika serikali mwaka wa 2022.

Alisema hilo litawezekana kwa vile yeye (Mbogo) yuko katika kundi ambalo linaunga mkono naibu wa Rais wakati Joho akiwa katika kundi pinzani.

“Kile ambacho tutaangalia sote ni nafasi ya Mpwani katika serikali itakayokuja. Hiyo inamaana kwamba Joho akipata Pwani itakuwa imepata na sisi pia Ruto akipata tutakuwa na mtu wetu ndani ambaye atakuwa naye hapo kwa kiti,” akasema Bw Mbogo.

Mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire ambaye aliandamana na Gavana Joho kumuona Moi alisema hakuna tatizo lolote kuhusiana na ziara hiyo.

Aidha alisema kuwa tayari katika Pwani, Magavana Amason Kingi na Hassan Joho wameeleza nia yao ya kuwania Urais ila wanafaa kuzunguka Kenya nzima na kutangaza sera zao.

You can share this post!

Raila amtaka Haji akome kuingiza siasa katika vita dhidi ya...

JAMVI: Mkakati mpya anaotumia Ruto kuhakikisha anatwaa...

adminleo