• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Kesi ya Mwilu kuamuliwa na majaji watatu

Kesi ya Mwilu kuamuliwa na majaji watatu

Na RICHARD MUNGUTI

HATIMA ya kesi ya kushtakiwa kwa na ufisadi kwa Naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu sasa iko mikononi mwa majaji watatu watakaoteuliwa na Jaji Mkuu David Maraga.

Na wakati huo huo Jaji Enock Chacha Mwita alisitisha kusikizwa kwa kesi ya ufisadi dhidi ya DCJ Mwilu mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi.

Bw Mugambi aliagizwa asubiri uamuzi wa jopo la majaji watatu watakaoteuliwa na CJ watakapotoa uamuzi.

Jaji Mwita aliamuru faili ya kesi ya DCJ Mwilu aliyowasilisha mahakama kuu ipelekwe kwa CJ awateue majaji watakaoamua ikiwa DPP alikosa kumshtaki naibu huyo wa rais wa Mahakama ya Juu au la.

Majaji hao watakaoteuliwa na Jaji Maraga wataamua ikiwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alitenda haki kuamuru DCJ Mwilu ashtakiwa angali kazini.

“Suala la kushtakiwa kwa DCJ Mwilu akiwa angali ofisini ni suala nyetu na muhimu kikatiba linalopasa kuamuliwa na majaji zaidi ya mmoja,” alisema Jaji  Enock Chacha Mwita aliyeamuru faili hiyo ipelekwe moja kwa moja hadi kwa CJ kuteua jopo la kuamua kesi hiyo.

Manaibu wa DPP Dorcus Oduor na Alexander Muteti. Picha/ Richard Munguti

Jaji Mwita alisema majaji hao wataamua ikiwa uhuru wa idara ya mahakama na utenda kazi wake umehujumiwa na kitengo cha afisi ya DPP iliyo chini ya afisi ya Rais kwa kuamuru jaji anayehudumu ashikwe na kushtakiwa kwa ufisadi.

DCJ Mwilu alipinga kukamatwa na kushtakiwa kwake akisema DPP ametumia mamlaka aliyopewa chini ya katiba alipoamuru ashikwe.

“Utararibu unaofuatwa ni jaji anayedaiwa amekiuka sheria ni kwanza tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama JSC imchunguze na ikimpata na hatia ipendekeze kwa Rais ateue jopo la kumchunguza na hatimaye itoe ripoti ikiwa ataondolewa kazini ndipo afunguliwe masahtaka,” DCJ Mwilu alilalama.

Naibu huyo wa rais wa Mahakama ya Juu alisema DPP alikaidi sheria kumtia nguvuni akiwa angali kazini na kumfikisha mahakamani.

DCJ Mwilu anaomba mahakama kuu ifutilie mbali kesi aliyoshtakiwa kwa kupokea mkopo kutoka kwa benki iliyofilisika ya Imperial. DCJ Mwilu anahoji makosa aliyofanya kukopa pesa kwa benki.

Aliomba mahakama kuu imzuie DPP kuendelea na kesi aliyomshtaki akisema lengo kuu dhamira kuu ni aondolewe kazini kwa njia ya aibu.

Wakili Nelson Havi (kulia , Seneta Okong’o Omogeni na mawakili wengine wanaomtetea DCJ Mwilu. Picha/ Richard Munguti

Naibu huyo wa CJ amesema kuwa anadhulumiwa kwasababu ya kuharamishwa kwa ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta na Mahakama ya Juu Septemba 1 2017.

Mahakama ya Juu ilifutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta baada ya kukubaliwa kwa kesi aliyoshtaki vinara wa Nasa Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kupinga matokeo ya  urais wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 8 2017.

DCJ Mwilu anasema katika kesi yake kuwa DPP hana uwezo kisheria kumfungulia Jaji anayehudumu kesi ya uhalifu na kwamba amekaidi vipengee vya Kifungu nambari 157 cha Katiba kinachompa mamlaka DPP kumfungulia mmoja mashtaka.

DCJ Mwilu anadai DPP anatumia vibaya mamlaka ya afisi yake.

Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo na DCJ , DPP kupitia kwa manaibu wake Dorcus Oduor na Alexander Muteti na Wakili Mkuu wa Serikali (SG) Kennedy Ogeto alipinga kesi hiyo ya DCJ Mwilu akisema haimbatani na sheria.

DPP aliomba majaji watatu au zaidi wateuliwe kusikiza kesi hiyo ya DCJ Mwilu akidai nguvu na mamlaka yake yamehojiwa na kwamba uamuzi wapasa kutolewa ikiwa alitenda haki au la kuamuru jaji huu mkuu ashtakiwe.

Akitoa uamuzi Jaji Mwita alisema masuala anayozua DCJ Mwilu ni mazito na yanahitaji kuamuliwa na majaji zaidi ya mmoja.

“Naamuru kesi hii ipelekwe kwa CJ ateue jopo la kuamua masuala nyeti na mazito ya kisheria kuhusu uwezo na nguvu za DPP kuamuru jaji anayehudumu akamatwe,” alisema Jaji Mwita,

You can share this post!

Wanahabari na mawakili waonywa dhidi ya kujadili kesi ya...

Uhuru atoa sababu za kupiga marufuku samaki wa Uchina

adminleo