• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Sikusema Uhuru aendelee kuongoza baada ya 2022 – Kalonzo

Sikusema Uhuru aendelee kuongoza baada ya 2022 – Kalonzo

Na WYCLIFFE MUIA

KINARA wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekanusha taarifa kuwa alipendekeza kuongezwa kwa muda wa kuhudumu wa rais, lakini akasema ataunga Rais Uhuru Kenyatta kuwa Waziri Mkuu iwapo atataka wadhifa huo baada ya mabadiliko ya katiba.

Bw Musyoka ambaye alikabiliwa na shutuma kali kutokana na kauli yake kuhusu muda wa utawala wa rais nchini, alisema kauli yake ilitafsiriwa vibaya na kamwe hawezi kuunga mkono kurefushwa kwa muhula wa urais.

“Mimi ni wakili wa masuala ya kikatiba na kutokana na hadhi ya kazi yangu siwezi kamwe kuunga kurefushwa kwa muda wa kutawala wa rais,” alisema Bw Musyoka katika mahojiano na runinga ya Citizen.

Makamu huyo wa Rais wa zamani alisema Rais Kenyatta ndiye rais bora zaidi nchini kufikia sasa kutokana na juhudi zake za kupambana na ufisadi, na kuwa atamuunga mkono iwapo atataka kuhudumu kama Waziri Mkuu baada ya kustaafu urais 2022.

“Uhuru ndiye rais bora zaidi na nafurahia kazi anayoifanya, anapaswa kuungwa mkono na kutiwa moyo. Iwapo bado atakuwa kinara wa chama cha Jubilee katika kinyang’anyiro cha 2022 na chama chake kishinde idadi kubwa ya wabunge, sharti atakayeshinda urais amteue kuwa Waziri Mkuu,” alisema Bw Musyoka.

“Kwa maoni yangu, naona tukiwa na serikali ya muungano baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 na iwapo hayo yatatokea huwezi kumuondoa Uhuru katika mpangilio wa serikali hiyo,” Bw Musyoka aliongeza.

Kwa mara nyingine Bw Musyoka alidokeza kuwepo na mpango wa kubuniwa kwa muungano mkubwa wa kisiasa unaojumuisha vyama vya Wiper, ODM, ANC na Ford Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Iwapo nitajipata nang’ang’ania wadhifa wa Waziri Mkuu pamoja na Uhuru, ni heri nimwachie na niwe naibu wake,” alisema Bw Musyoka.

Hata hivyo, kauli ya Bw Musyoka inatofautiana na msimamo wake wa kuwa sharti awanie urais 2022.

Bw Musyoka alitetea kauli yake ya kuwa ‘mtu wa mkono wa rais’ akisema ilieleweka vibaya na kutumiwa vibaya na maadui wake wa kisiasa.

“Nilichomaanisha ni kuwa nitamuunga mkono ndugu yangu Uhuru katika juhudi zake za kuunganisha nchi na kupigana na ufisadi. Bila shaka kauli hiyo ilichukuliwa vingine na watu ambao wanatafuta umaarufu wa kisiasa kwa kunikashifu na nimewazoea,” alisema Bw Musyoka.

Kuhusiana na mgawanyiko unaoshuhudiwa katika chama chake cha Wiper, Bw Musyoka alisema hakuna uasi wowote katika chama chake na kuwa ‘kelele’ zinazosikika ni baadhi ya viongozi wanaojitafutia makuu.

Magavana Prof Kivutha Kibwana (Makueni), Charity Ngilu (Kitui) na Dkt Alfred Mutua (Machakos) wamekuwa wakimshutumu Bw Musyoka kwa uongozi duni wanaodai hausaidii jamii ya Wakamba.

Hata hivyo, Bw Musyoka alisema magavana hao wana uhuru wa kuwania urais bila kumtumia kama kizuizi cha azma yao.

Bw Musyoka alimtaka Prof Kibwana kujiuzu kama mwenyekiti wa Wiper bila kutafuta vijisababu vya kutimuliwa.

You can share this post!

MGOMO: Serikali yavuna matunda ya kukaidi mahakama

Chimbuko la kushtua kuhusu Valentino Dei

adminleo