• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Arsenal yazima makali ya United kutua nne-bora EPL

Arsenal yazima makali ya United kutua nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

ARSENAL waliweka hai matumaini ya kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora baada ya kukizamisha chombo cha watani wao Manchester United uwanjani Emirates.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer kupoteza katika EPL tangu aaminiwe kushikilia mikoba ya Man-United baada ya Jose Mourinho kutimuliwa.

Kiungo Granit Xhaka aliwafungulia Arsenal ukurasa wa mabao katika dakika ya 12 kabla ya mvamizi Pierre-Emerick Aubameyang kupachika la pili.

Bao la Aubamenyang ambaye ni raia wa Gabon lilikuwa zao la Fred kumchezea visivyo fowadi Alexandre Lacazette wa Arsenal.

Romelu Lukaku na Fred walipoteza nafasi nyingi za wazi katika mchuano huo uliomweka kipa wa Arsenal Bernd Leno katika ulazima wa kufanya kazi nyingi za ziada.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne kwa alama 60, moja pekee nyuma ya Tottenham Hotspur.

Man-City wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa pointi 74, moja zaidi kuliko Liverpool ambao wanajivunia pengo la alama 12 kati yao na Spurs.

Man-United waliteremka hadi nafasi ya tano kwa alama 58, moja mbele ya Chelsea ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi 30 ambazo zimepigwa na wapinzani wao wengine ndani ya mduara wa tano-bora.

Kujinyanyua

Arsenal walijibwaga katika mchuano huo wakipania kujinyanyua siku tatu baada ya chombo chao kuyumbishwa kwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Rennes katika Ligi ya Uropa.

Kinyume na matarajio, Man-United walitazamiwa kuendeleza ubabe wao dhidi ya Arsenal hasa baada ya kuwabandua PSG kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Nafuu zaidi ni kwa Arsenal ambao kwa sasa wamecheza dhidi ya washindani wao wakuu katika vita vya kupigania nafasi nne za kwanza jedwalini.

Kinyume na Arsenal, Man-United wanakabiliwa na mitihani migumu dhidi ya Everton, Man-City na Chelsea katika jumla ya mechi nane zilizosalia msimu huu.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Rennes ya Ufaransa katika mchuano wa mkondo wa pili wa Ligi ya Uropa mnamo Alhamisi uwanjani Emirates, Uingereza.

Kwa upande wao, Man-United watakuwa wageni wa Wolves mnamo Jumamosi katika robo-fainali ya kuwania ubingwa wa Kombe la FA.

You can share this post!

NI KISASI: Atletico kwenye mizani ya Juventus huku City...

Bandari wadhibiti usukani, Ingwe na Vihiga zikipaa KPL

adminleo