• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Aisha Jumwa alazwa kwa mshtuko wa kulaki mwili wa kaka yake

Aisha Jumwa alazwa kwa mshtuko wa kulaki mwili wa kaka yake

Na CHARLES LWANGA

AFYA ya Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa inaendelea kuimarika tangu alazwe hospitalini baada ya kupokea mwili wa kakake Uwanja wa ndege wa Mombasa aliyefairiki nchini Uchina.

Bi Jumwa alikimbizwa hospitalini Mombasa baada ya afya yake kudhoofika muda mchache baada ya kuona mwili wa kakaye Jumaa Karisa, jambo lililomlazimu alazwe katika chumba cha watu mahututi (ICU).

Hii si mara ya kwanza mbunge huyo amelazwa hospitalini baada ya afya yake kudhoofika.

Ripoti za kuaminika ziliambia Taifa Leo kuwa Bi Jumwa amekuwa akipambana na hali ya afya yake baada ya kufanyiwa upasuaji wa mbavu miaka miwili iliyopita wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi.

Mwakilishi wa wanawake Getrude Mbeyu ambaye pamoja na Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori walihudhuria matanga ya kakake Jumwa, aliambia Taifa Leo kuwa mbunge huyo hangeweza kuhudhuria kwa sababu ya uchovu.

“Alilalamikia uchovu na akakimbizwa hospitali ambapo alilazwa,” alisema na kuongeza kuwa “ingawaje hali yake imeimarika na huenda akatoka hospitalini leo.”

Bi Jumwa ambaye anajulikana kwa ujasiri wake kisiasa na kiongozi mwenye azma ya kumrithi Gavana Amason Kingi mwaka wa 2022 pia hakuhudhuria mkutano wa wabunge wa pwani ulioitishwa na Bw Kingi katika hoteli ya Sun N Sand mnamo Jumamosi.

Bi Jumwa ambaye amekuwa akigonga vinya vya habari kutokana na uamuzi wake wa kuunga mkono azama ya urais ya Naibu Rais William Ruto mwaka wa 2022, hakuhudhuria matanga ya kakake nyumbani kwao Takaungu eneo bunge la Kilifi Kaskazini Ijumaa iliyopita.

Katika mazishi, Bi Mbeyu aliomba msamaha kwa niaba ya Bi Jumwa kwa kutohudhuria matanga na akasema mbunge huyo amehuzunishwa sana na kifo cha kakake.

“Tulishtuka tulipopokea ripoti za kifo ya Jumaa na Bi Jumwa amekuwa mbioni tangu habari hizo zimfikie hadi alipoupokea mwili wake katika uwanja wa ndege, ninadhani hayajakuwa vizuri kwa Bi Jumwa ambaye sasa ni mgonjwa,” alisema.

Bw Richard Mitingi, ambaye ni maneja wa Bi Jumwa alisema Bi Jumwa amekuwa akifanya kazi nyingi na alipelekwa hospitali kwa ajili ya uchovu.

Katika mkutano wa wabunge Jumamosi iliyopita ambayo wabunge wakiongozwa na Gavana Kingi walisema wanafuatilia kwa makini jinsi chama cha ODM kimemwandikia Bi Jumwa na Bw Dori barua ya kujieleza ni kwa nini wasichukuliwe hatua ya kinadhamu kwa kumuunga mkono Bw Ruto.

You can share this post!

Agizo la HELB laibua hofu katika Chuo Kikuu cha Moi

Komeni kutumia bunge kulipiza visasi vya kisiasa, arai...

adminleo