• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Gareth Bale aangika daluga zake katika ulingo wa soka akiwa na umri wa miaka 33

Gareth Bale aangika daluga zake katika ulingo wa soka akiwa na umri wa miaka 33

Na MASHIRIKA

NAHODHA wa timu ya taifa ya Wales, Gareth Bale, ameangika daluga zake katika ulingo wa soka akiwa na umri wa miaka 33.

Nyota huyo ambaye amewajibikia Wales mara nyingi zaidi ndiye anashikilia rekodi ya ufungaji bora katika historia ya kikosi hicho. Alitangaza kustaafu kwake kupitia mitandao ya kijamii.

Bale, ambaye ni mshindi mara tano wa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akichezea Real Madrid, ndiye mwanasoka bora kuwahi kujivuniwa na Wales.

“Baada ya kuwazia kwa makini, nimeamua kustaafu katika ulingo wa soka kwenye ngazi ya klabu na kimataifa,” akasema Bale.

“Najihisi mwenye bahati kubwa kuwa miongoni mwa wanasoka ambao wamefikia ndoto zao kitaaluma wakishiriki mchezo wanaoupenda,” akaongezea.

Sogora huyo ambaye ni mzawa wa Cardiff, alijiunga na Tottenham Hotspur baada ya kuagana na Southampton. Alijiunga baadaye na Real katika uhamisho ulioweka rekodi ya dunia kabla ya kujiunga na Los Angeles FC ya Major League Soccer (MLS) nchini Amerika mnamo Juni 2022.

Alikuwa nahodha wa Wales alipoongoza kikosi hicho kufuzu kwa fainali za Euro 2016 na 2020 na akasaidia pakubwa timu hiyo kutinga fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar kwa mara ya kwanza tangu 1958. Anaangika daluga zake akijivunia kufungia Wales mabao 41 kutokana na mechi 111.

Akiwa Spurs, Bale aliwahi kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka mnamo 2010-11 na 2012-23 kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Real kwa kima cha Sh11.9 bilioni mnamo Septemba 2013.

Akivalia jezi za Real, Bale aliongoza miamba hao kunyanyua mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na matano ya UEFA. Hakuna mchezaji mwingine yeyote kutoka Uingereza amewahi kufikia rekodi hiyo. Bale alizolea Real pia makombe matatu ya Kombe la Dunia kwa vilabu, matatu ya Uefa Super Cup na ubingwa wa Spanish Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto aahidi kuwa rekodi za ardhi Pwani zitawekwa kwa mfumo...

Chuo cha kiufundi chajengwa mjini Ruiru

T L