• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Utata wa kesi ya mvulana wa miaka 13 akinajisi msichana wa miaka 4   

Utata wa kesi ya mvulana wa miaka 13 akinajisi msichana wa miaka 4  

 

NA TITUS OMINDE

MVULANA wa miaka 13 anayekabiliwa na mashtaka ya unajisi kinyume na sheria ya makosa ya ngono ya 2006 atajua hatima yake Juni 6, 2023 baada ya mahakama ya Eldoret kuahirisha kesi yake.

Mnamo Jumatano, Mei 31, 2023 hakimu mwandamizi wa Eldoret Caroline Waltima aliahirisha kusomewa mashtaka akisubiri kuteuliwa kwa wakili wa kumwakilisha mshtakiwa kwa vile yeye ni mtoto.

“Kwa kuwa mhusika ana umri wa miaka 13, ninaahirisha kesi hii hadi wakili wa kujitolea atakapoagizwa kuwakilisha mshtakiwa. Kesi hiyo itatajwa Juni 6,” aliamuru Hakimu.

Shtaka lilisema kuwa mshtakiwa ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Msingi katika Kaunti Ndogo ya Moiben alitenda kosa hilo Mei 19, 2023.

Mshtakiwa alidaiwa kumnajisi mtoto huyo walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka shuleni.

Mlalamishi na mshtakiwa wote wanasemekana kufahamiana kwa kuwa wanaishi mtaa mmoja.

Awali afisa wa uchunguzi alikuwa amempeleka msichana huyo hospitalini ambapo alilazwa kwa wiki moja kabla ya kuruhusiwa kuondoka baada ya kupata nafuu.

Mshtakiwa alikamatwa Mei 29, 2023 baada ya upelelezi kukamilika.

Kulingana na wakili wa watoto kutoka Eldoret, Lauren Isiaho, kesi kama hiyo haifai kufuata mchakato mzima wa kesi za unajisi kwa kuwa inahusisha watoto wanaohitaji ulinzi na kutunzwa.

Bi Isiaho alisema jambo la dharura zaidi linalohitajika katika hali hiyo, ni kuwaokoa watoto wote wawili na kuwapa mwongozo na ushauri chini ya uangalizi wa maafisa wa huduma za watoto.

Wakili huyo alisema kesi za aina hiyo pia zinahitaji michango ya maafisa wa uangalizi kutoa ripoti ya mienendo ya mshtakiwa ili kupata mwongozo wa namna ya kushughulikia suala hilo katika mfumo wa kisheria kwa kurejelea tabia ya mshatakiwa.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Sheria ya Watoto ya 2022 inabainisha jinsi masuala kama hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa mtazamo wa kisheria.

“Hii ni kesi ambayo inahusisha watoto wawili na haiwezi kukabiliwa kikamilifu kama kesi zingine za unajisi lakini badala yake mahakama inapaswa kuzingatia sheria ya watoto ya 2022,” alisema Bi Isiaho.

Kesi hiyo itatajwa Juni 6.

 

  • Tags

You can share this post!

Vituko: Sonko athibitisha ‘blingi’ zake si feki

Kamene na Bonez washangaza wakidai hutumia mswaki mmoja  

T L