Mapambano ya kurithi Tsvangirai yaanza kutikisa chama cha MDC

Mwili wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Bw Morgan Tsvangirai watolewa kwa ndege tayari kwa mazishi yaliyofanyika Februari 21, 2018. Picha/ Mashirika

Na AFP

KIFO cha kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, kimeibua mvutano kuhusua anayefaa kumrithi katika Chama cha Movement for Democratic Change (MDC) alichokiongoza, hali ambayo inatishia kugawanya chama hicho.

Mzozo huo wa mamlaka ulishuhudiwa hata kabla ya Tsvangirai kuzikwa Jumanne, wakati naibu rais wa chama hicho, Bw Thokozani Khupe, alipozomwa wakati wa mazishi, kwa mujibu wa afisa wa chama, Bw Douglas Mwonzora.

Zimbabwe imepanga kufanya uchaguzi mkuu mwezi Julai na Rais Emmerson Mnangagwa, anayeongoza chama tawala cha ZANU-PF aliahidi uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika kwa heshima ya marehemu.

Maelfu ya watu walikusanyika kumpa buriani kigogo huyo wa kisiasa ambaye ni mmoja wa viongozi wa upinzani waliothaminiwa zaidi barani Afrika.

“Tunasherehekea maisha ya shujaa,” alisema kaimu rais wa MDC, Bw Nelson Chamisa.

Tsvangirai ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa utawala wa kiimla wa aliyekuwa rais Robert Mugabe, alifariki Jumatano iliyopita akiwa na umri wa miaka 65 katika hospitali moja ya Afrika Kusini ambako alikuwa anatibiwa saratani ya utumbo.

Mwili wake ulisafirishwa hadi mazishini kwa helikopta ya kijeshi, ukiwa umeandamana na mamake, Bi Mbuya Tsvangirai.

Maelfu ya waombolezaji walivumilia mvua na kukusanyika katika boma lake lililo Buhera, kilomita 220 kusini mwa mji mkuu wa Harare. Naibu Rais wa Zimbabwe, Oppah Muchinguri, pia alihudhuria pamoja na mabalozi wa Amerika na Ulaya.

 

Kilio

Watu wengi walivaa tisheti nyekundu zenye picha ya Tsvangirai huku wakipuliza firimbi huku wengine wakilia.

Ingawa azimio la Tsvangirai kumng’atua Mugabe mamlakani kupitia kwa uchaguzi lilizimwa katika chaguzi kadhaa, alifanikiwa kushuhudia Mugabe akijiuzulu Novemba mwaka uliopita baada ya kutawala kiimla kwa miaka 37.

Mugabe na mke wake, Grace, walituma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu.

Tsvangirai alimshinda Mugabe katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa urais mwaka wa 2008 lakini kulingana na tume ya uchaguzi, hakufikisha idadi ya kura kumwezesha kutangazwa Rais.

Alikataa kushiriki marudio ya uchaguzi baada ya ghasia kutokea ambapo wafuasi wake wasiopungua 200 waliuawa.

Kiongozi wa zamani wa upinzani, Bw Arthur Mutambara, ambaye alikuwa naibu wa Tsvangirai katika serikali ya mseto, alisema Tsvangirai ndiye alikuwa rais halisi wa Zimbabwe.

“Alikamatwa akapigwa. Wanachama wa ZANU-PF pia wako hapa, wao ndio walimuua Morgan Tsvangirai,” akasema.